Sheikh Aliyetuhumiwa kwa Ugaidi Afariki Mbele ya Jaji

 


Sheikh Said Ukatule, aliyekuwa mahabusu ya Gereza Kuu la Ukonga, jijini Dar es Salaam, alikokuwa akishikiliwa na serikali kwa mashitaka ya ugaidi, amefariki dunia ghafla mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Salma Maghimbi.


Taarifa iliyotolewa leo Jumanne, tarehe 7 Machi 2023 na Katibu Mkuu wa Shuraa ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, zinaeleza kuwa Sheikh Ulatule, alifariki dunia mbele ya Jaji huyo Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, tarehe 4 Machi 2023.


Kabla ya kukutwa na mauti, Sheikh Ulatule alikuwa akijaribu kumueleza Jaji Maghimbi, matatizo wanayopitia wafungwa na mahabusu katika gereza hilo.


“Tarehe 4 Machi 2023, Jaji Magimbi alifanya ziara katika Gereza la Ukonga, baada ya kuwasikiliza wafungwa iliwadia zamu ya mahabusu wakiwamo waislamu wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya ugaidi.


“Katika kikao hicho, Sheikh Ulatule aliinua mkono na Jaji Maghimbi alimpa fursa ya kueleza shida zake, hata hivyo hakuweza kusema lolote bali alianguka na kufariki dunia papo hapo mbele ya Jaji, wafungwa, mahabusu na maofisa wa Magereza,” imeeleza taarifa ya Sheikh Ponda.


SHEIKH APOTEZA MAISHA MBELE YA JAJI Sheikh Saidi (80), (kesi Ugaidi) akilalamika mbele ya Mh. Magimbi Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu kwa kuwekwa gerezani yeye na wenzake miaka mingi alianguka na kufariki. Tukio limetokea gerezani trh 4/3/23. Tunalaani mfumo huu kandamizi kwa raia. pic.twitter.com/dOYZSuCM5z


— Shekh Ponda Issa Ponda (@SheikhPonda) March 6, 2023


Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya kifo cha Sheikh Ulatule, tarehe 6 Machi 2023, taasisi yake iliruhusiwa kwenda Gereza la Ukonga kufanya mazungumzo na uongozi wa gereza hilo, ambapo ulimteua afisa mmoja kushirikiana nao katika uchunguzi wa sababu za kifo cha sheikh huyo na kukabidhiwa mwili wa marehemu.


Amesema, uchunguzi wa mwili huo ulifanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo taarifa ya daktari ilibainisha kwamba marehemu alifariki dunia baada ya kupata mshtuko wa moyo ambao ulishindwa kufanya kazi.


Ameongeza, “Shura walikabidhiwa mwili saa 11.00 jana jioni na kuhifadhi katika chumba cha maiti kilichopo katika makaburi ya Mwinyimkuu, Magomeni, Dar es Salaam.”


Sheikh Ponda amesema, mwili wa Sheikh Ulatule utapelekwa nyumbani kwa mwanae maeneo ya Kitunda jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya taratibu mazishi zitakazofanyika leo tarehe 7 Machi 2023.


Kupitia taarifa hiyo, Sheikh Ponda ameiomba Serikali iharakishe usikilizaji wa mashauri ya watuhumiwa wa ugaidi yanayowakabili masheikh waliosalia mahabusu kwa zaidi ya miaka sita hadi kumi.


Hata hivyo, kumekuwa na juhudi za makusudi zinazofanywa na serikali, kupitia Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP), tangu Mei mwaka juzi, kufuata au kuwaachia kwa masharti maalum, baadhi ya watuhumiwa wa ugaidi, tangu Rais Samia Suluhu Hassan, aingie madarakani Machi 2021.


Ofisi ya DPP na mkurugenzi mwenyewe wa mashitaka, Sylvester Mwakitalu, wamefanya mazungumzo na Masheikh wanaokabiliwa na tuhuama za ugaidi, ikiwemo viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar, kabla ya kuwaachia huru 16 Juni 2021.


DPP alifanya mazungumzo na Masheikh hao Jumamosi ya tarehe 12 Juni 2012; mazungumzo yao yalichukua muda wa saa mbili na nusu.


Masheikh wa Uamsho walikamatwa na kuzuiliwa gerezani tangu mwaka 2014 na kwamba takribani masheikh 51 wa Uamsho walikuwa wakisota mahabusu tangu walipokamatwa katika nyakati tofauti mwaka 2012.


Walikuwa wakikabiliwa na kesi ya Jinai Na. 121/2021, katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad