UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa dakika 180 za mechi zao za Uwanja wa Mkapa watakomalia kushinda mechi zote ili wafufue matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba kwenye hatua ya makundi ilianza kwa kupoteza Februari 11 ubao wa Uwanja wa General Lansana Conte uliposoma Horoya 1-0 Simba, Uwanja wa Mkapa uliposoma Simba 0-3 Raja Casablanca ilikuwa Februari 18 na Uwanja wa St Mary’s Februari 25 uliposoma Vipers 0-1 Simba huu ulikuwa ushindi wao wa kwanza.
Kwenye kundi C Simba ipo nafasi ya tatu baada ya kukusanya pointi tatu vinara ni Raja Casablanca wenye pointi tisa wao wameshinda mechi zao zote.
Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kuwa Vipers hawatakuwa na bahati Uwanja wa Mkapa hata Horoya nao wasahau.
“Vipers wanakuja Uwanja wa Mkapa hakika hawatakuwa na bahati tutawapelekea balaa zito ambalo watakutana nalo kisha tutachukua pointi tatu muhimu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Hapo wanakuja Horoya, walitufunga kwao mchezo wa kwanza na kupoteza furaha yetu sasa tunawaambia karibu Dar hakika ni sehemu yetu kuchukua pointi tatu lazima tutawapelekea pumzi ya moto na pointi tatu tutabaki nao.
“Hapo tutakuwa tumekusanya pointi sita ni nyingi kweli kwetu lazima tutazipambania kisha mchezo wetu wa mwisho utakuwa ni wa kujitoa kwa kila mchezaji kusaka pointi tatu ugenini dhidi ya Raja Casablanca ambao walitufunga mchezo uliopita,” alisema Ally.
Mchezo wa Simba dhidi ya Vipers unatarajiwa kuchezwa kati ya Machi 7 na ule dhidi ya Horoya unatarajiwa kuchezwa kati ya Machi 18.
KUNDI LA SIMBA CAF
P W D L GF GA Pts
1.Raja CA 3 3 0 0 10 0 9
2.Horoya 3 1 1 1 1 2 4
3.Simba 3 1 0 2 1 4 3
4.Vipers 3 0 1 2 0 6 1
RATIBA YAO
Machi 7, 2023
Simba v Vipers saa 1:00 Usiku
Machi 18, 2023
Simba v Horoya saa 1:00 Usiku
Machi 31, 2023
Raja Casablanca v Simba