TIMU ya Simba imefuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya ya Guinea katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Shujaa katika mchezo huu ni Clatous Chama aliyefunga matatu 'Hat-Trick' dakika ya 10, 36 na 70 huku Jean Baleke akifunga mawili dakika ya 32, 65 na Sadio Kanoute akifunga pia mawili dakika ya 55 na 87.
Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huu.
Huu ni ushindi wa kwanza mkubwa kwa Simba katika hatua hii ya makundi baada ya kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Vipers SC kwenye michezo miwili iliyopita iliyopigwa jijini Uganda na Dar es Salaam.
Chama anakuwa ni mchezaji wa kwanza wa Simba katika hatua hii ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kufunga 'Hat-Trick' ikiwa ni siku chache tu tangu nyota huyo achaguliwe na CAF kuwa mchezaji bora wa wiki.
Simba inakuwa ni timu ya pili kutinga hatua ya robo fainali katika historia ya mashindano ya Klabu Afrika baada ya kupoteza michezo miwili ya mwanzo ya hatua ya makundi.
Timu ya kwanza kufanya hivyo kabla ya Simba ilikuwa ni Es Setif ya Algeria ambayo mwaka 2018 ilipoteza mchezo wa kwanza wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe kwa mabao 4-1.
Baada ya hapo ilichapwa bao 1-0 na MC Alger kwenye mechi ya pili ila ilitinga robo fainali baada ya kuvuna pointi nane katika michezo minne ya mwisho na mwaka huo iliishia hatua ya nusu fainali.
Desemba 23, 2018, Chama anakumbukwa zaidi wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana ya Zambia ambapo alifunga bao la tatu na la ushindi dakika ya 88 na kuifanya Simba kushinda 3-1.
Katika ushindi huo uliifanya Simba kufuzu hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 4-3 licha ya mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Zambia kuchapwa 2-1.
Februari 6, 2021 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilishinda mabao 4-0 dhidi ya FC Platinum huku Chama akifunga bao la mwisho lililoipeleka timu hiyo hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya ugenini kupoteza bao 1-0.
Simba imefuzu rasmi baada ya kufikisha pointi tisa nyuma ya vinara Raja Casablanca kutoka Morocco iliyokuwa ya kwanza kutinga robo fainali kwenye kundi 'C' kufuatia kufikisha pointi zake 13.
Mchezo mwingine wa kundi hili uliopigwa jijini Kampala nchini Uganda, Vipers imetoka sare ya bao 1-1 na Raja Casablanca.