Dar es Saalam. Timu ya taifa ya Tanzania imeibuka na ushindi wa bao 1-0, ugenini mbele ya Uganda katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon 2023), zitakazofanyika nchini Ivory Coast mwaka huu.
Katika mechi hiyo ya kwanza kwa kocha mpya wa Stars, Adel Amrouche bao pekee na la ushindi kwa Stars lilifungwa na Simon Msuva dakika ya 68 akimalizia pasi safi ya Dickson Job aliyekuwa aliyecheza eneo la beki wa kulia.
Katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo, timu zote zilicheza kwa kushambulia kwa kushitukiza lakini hadi dakika 45 zinamalizika matokeo yalikuwa 0-0.
Uganda iliingia kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko matatu ya pamoja wakitoka Farouk Miya, Fahad Bayo, na Siraje Ssentamu na kuingia Isma Mugulusi, Steven Sserwadda, ambaye aliumia dakika 10 baadae na kutolewa nafasi yake ikichukuliwa na Allan Okello.
Mabadiliko hayo yaliyolenga kushambulia, yalilipwa na kocha wa Stars Amrouche ambapo dakika ya 57 naye alimtoa mshambuliaji Hamis Said Jr na kumuingiza Abdul Seleman ‘Sopu’ mabadiliko yaliyoinufaisha zaidi Stars na kupata bao la kuongoza.
Baada ya bao la Msuva, Stars iliendelea kumiliki mpira kwa nidhamu huku Uganda ikikaba na kufanya mashambulizi ya kushitukiza ambayo mengi yalizuiwa na ukuta wa Stars chini ya Bakari Mwamnyeto.
Uganda baada ya kupata ugumu upenya ngome ya Stars ilifanya mabadiliko tena dakika ya 71 kwa kumtoa nahodha wao, Emmanuel Okwi na kuingia Mato Kassim na Stars ikajibu mapigo dakika ya 80 akitoka Mudathir Yahya na kuingia Feisal Salum ‘Fei Toto’ kisha dakika ya 85 akaingia Kelvin John kuchukua nafasi ya Msuva aliyeumia.
Mabadiliko hayo hayakubadili matokeo na dakika 90 kumalizika kwa Stars kuibuka na ushindi ugenini.
Matokeo hayo yameifanya Stars kupaa hadi nafasi ya pili kwenye kundi F na pointi nne, nyuma ya vinara Algeria walioshinda mechi zote tatu huku Niger ikikaa nafasi ya tatu na pointi mbili na Uganda ikiburuza mkia na pointi moja tu.
Stars imebakiza mechi tatu za uamuzi ambapo Jumanne Machi 28 mwaka huu itaikaribisha Uganda katika mechi ya marudiano itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na baada ya hapo itawakaribisha Niger ambayo katika mechi ya kwanza ililazimishwa sare ya bao 1-1 kwao na Algeria iliyoshinda 2-0 nyumbani.