IKICHEZA mbele ya mashabiki kibao Dimba la Mkapa jijini Dar, jana Machi 28, 2023 Taifa Stars ilishindwa kuwapa furaha baada ya kuruhusu bao dakika za mwisho mbele ya Uganda ‘The Cranes’ katika mchezo wa raundi ya nne ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa Afrika.
Stars ambayo ilikuwa inapewa nafasi ya kushinda mchezo huo, ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huku ikikosa mabao kadhaa ya wazi kupitia kwa washambuliaji wake wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta.
Alikuwa ni Rodgers Mato aliyepeleka kilio dakika ya 90 wakati wengi wakidhani mechi ingeisha suluhu lakini bao hilo limewafanya sasa Stars kuhakikisha inashinda michezo yake miwili iliyobaki dhidi ya Algeria na Niger ambayo utapigwa Juni na Septemba mwaka huu jijini Dar huku wakiombea Uganda wapate matokeo mabaya.
Kwa matokeo hayo, Stars kwenye msimamo wa Kundi F inakuwa ya pili ikiwa imelingana kila kitu na Uganda walio nafasi ya tatu ambapo kila mmoja amecheza mechi nne, ushindi moja, sare moja na kufungwa miwili, mabao ya kufunga ni mawili na kufungwa manne kila mmoja.
Kuna uwezekano mkubwa mechi za mwisho ndizo zitakazoamua timu itakayoungana na Algeria kwenda kushiriki Afcon mwaka huu.
UMEME WATIBUA HALI YA HEWA
Katika hali isiyokuwa ya kawaida dakika ya 38 mwamuzi alilazimika kusimamisha mchezo huo kutokana na mwanga hafifu uliotokana na baadhi ya taa kuzima.
Hali hiyo ilisababisha mechi isimame kwa zaidi ya dakika 20 kusubiri matengenezo na hali ilipokuwa sawa mechi ilirejea kwa kasi.
RATIBA YAO
Juni 12, 2023
Uganda vs Algeria
Tanzania vs Niger
Stori Na Joel Thomas, Gazeti la Championi