Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni, watu wanne walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji.
Machi 19, 2023 mvua kubwa ilionyesha maeneo mbalimbali na kusababisha madhara ikiwemo biashara kusimama na baadhi ya barabara kutopitika.
Mtambule ameyasema hayo leo Machi 25, 2023 Kata ya Mbweni, wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo alipotembelea Mto Mpiji.
Amesema maeneo mengi ya Dar es Salaam hasa Kinondoni jiografia yake ni ya milima na mabonde lakini wakati mwingine watu wamejitokeza na kuanza kuchimba mchanga kinyume na utaratibu.
"Maeneo mengi yameathirika na mvua kutokana na uharibifu wa mazingira, mfano ni mvua zilizonyesha hivi karibuni watu wanne walifariki kwa kusombwa na maji," amesema Mtambule.
Amebainisha kuwa uchimbaji wa mchanga kiholela hasa maeneo ya Mabwepande, Mbweni na Bunju umechangia wananchi kukosa huduma za kijamii hasa pale mvua zinaponyesha.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbweni, Mpiji Moses Magogwa amesema vitendo vya uharibifu kwenye mtaa huo vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku.
Amesema wakati mwingine wamekuwa wakichimba usiku hata wanapotoa taarifa hadi mamlaka zinazohusika zifike wahusika wanakuwa wameshaondoka.