UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Ni kweli Tshabalala na Kapombe wamezeeka?





SIJAMUELEWA kocha wa Taifa Stars. Sijamuelewa kabisa Adel Amrouche. Nimeshangaa sana kuona timu yetu ya Taifa ‘Taifa Stars’ inaitwa bila kuwa na majina ya Mohammed Hussein, Aboubakary Salum na Shomary Kapombe. Kwenye kizazi hiki Kapombe na Mohammed ndiyo mabeki wetu waliocheza michuano mikubwa zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.

Ndiyo wachezaji ambao hata pale Simba wageni wote wameshindwa kuwatoa kwenye nafasi zao. Ndiyo wachezaji bora kwenye eneo la ulinzi wa pembeni. Sidhani kama kocha wetu mpya Amrouche ameshauriwa vizuri.

Sidhani kama wasaidizi wake na Kurugenzi ya Ufundi kama wamefanya kazi yao sawasawa.

Tanzania inataka kufuzu kwa mara ya tatu kwenye michuano ya Afcon, lakini inakwenda vitani bila askari wake wenye uzoefu. Tanzania inakwenda vitani bila wachezaji wake bora wa kulia na kushoto kwenye eneo la kujilinda.


Amrouche amejiweka mwenyewe kwenye mtego. Hakuna kitu kingine anachoweza kuwapa Watanzania wakamuelewa tofauti na kufuzu fainali za Afcon. Taifa Stars ikishindwa kupata matokeo mazuri, tayari kocha ameshawapa watu sababu.

Kapombe na Tshabalala bado tunawahitaji sana kwenye kikosi cha Taifa Stars. Nilidhani Amrouche amepata nafasi ya kutazama hata mechi zetu tatu za Stars zilizopita.

Nilidhani Amrouche amepata nafasi hata kutazama mechi za Simba dhidi ya Vipers ya Uganda kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Sidhani kama kocha amewatazama vizuri wachezaji hawa. Sidhani kama alipata nafasi. Tumeita wachezaji wengi sana wanaocheza nje ya Tanzania, lakini tumepata nafasi ya kufuatilia maendeleo yao huko nje hivi karibuni? Sina hakika.

Mchezaji anaweza kuwa anacheza soka nje ya Tanzania, lakini kwa kiwango cha kawaida. Nadhani ni muda sahihi sasa kwa kocha kuanza kutembea na kuwaona wachezaji wakiwa na klabu zao. Kuna muda nahisi tunawaita tu. Kuna muda ni kama tunawaonea aibu. Timu ya taifa sio mahali ambapo kila mtu anacheza. Ni mahali ambapo walio bora tu ndiyo wanaitwa. Kumuacha Kapombe na Tshabalala sidhani kama tumewatendea haki. Kumuacha Tshabalala na Kapombe sidhani kama tumejitendea haki hata sisi wenyewe. Wachezaji wa aina hii huwa hawaachwi tu kama mahindi. Huwa kunakuwa na sababu za msingi ambazo wananchi wanapawa kuelezwa. Mohammed Hussein na Shomary Kapombe ni wachezaji wakubwa huwezi kuwaacha tu bila walau kuwajuza Wananchi sababu za kuwatema kikosini.

Kama kocha mgeni ameweza kumuona David Luhende akiwa Kagera Sugar hawezi kushindwa kumuona Tshabalala pale Simba.

Ukitazama vizuri kikosi chetu unapatwa na wasiwasi mkubwa juu ya leo na kesho yetu. Kapombe anapaswa kucheza leo, ameachwa. Clement Mzize anapaswa kucheza kesho, ameachwa. Tunahitaji matokeo mazuri leo lakini tunahitaji kuandaa vijana wa kesho.


Kwa kiwango ambacho Mzize amekionyesha hivi karibuni akiwa na Yanga nilidhani anastahili kuitwa timu ya taifa. Amrouche ana kazi kubwa. Kitu pekee ambacho kitamuweka salama ni ushindi.

Haya malalamiko yote huwa yanazimwa na matokeo mazuri. Hakuna mtu atamkumbuka Tshabalala kama Uganda watafungwa. Hakuna mtu atasikitika kuachwa kwa Kapombe kama timu itashinda. Unapoacha wachezaji wakubwa kama hawa ni kama kujivisha mabomu. Muda wowote Amrouche anaweza kulipuka. Ni muda wa kuanza kuwaandaa kina Kelvin John na Mzize. Hawa vijana kucheza na gwiji kama Mbwana Samatta inasaidia sana kwenye ukuaji wa vijana wadogo.

Ni kweli Kapombe na Tshabalala wamezeeka? Majibu yote nadhani yako kwa kocha wetu mkuu, Amrouche. Nimetazama eneo la kiungo sijaona jina la Aboubakary Salum “Sure Boy”.

Huyu nadhani alistahili pia kuwa sehemu ya kikosi. Huyu ni kiungo fundi kutoka kwa Wananchi ambao wamekuwa bora sana siku za hivi karibuni.


Kocha wetu Amrouche amefanya uamuzi mgumu sana ambao anatakiwa kueleweka kwa kufuzu kwa michuano ya Afcon.

Timu yetu iliyoitwa imeacha wachezaji wengi ambao wamekuwa kwenye kiwango bora siku za hivi karibuni.

Zawadi pekee ambayo Watanzania wanatakiwa kupewa na Kocha Amrouche ni ushindi dhidi ya Uganda. Wachezaji kama Kapombe, Tshabalala, Mzize na Sure Boy wote walistahili kuitwa Taifa Stars, lakini tunaheshimu uamuzi wa kocha.

Uganda ndilo taifa lililoshiriki michuano ya Afcon mara nyingi zaidi kuliko nchi yoyote ile kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Tuna mechi ngumu sana, lakini kocha wetu anaweza kutupigania. Mara ya mwisho tulipofuzu kwa fainali za Afcon tuliifunga pia Uganda. Kocha kafanya uamuzi mgumu, lakini naamini tutapata matokeo mazuri kwa kuifumua Uganda. Kila la heri Taifa Stars.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad