Moshi. Baada aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, mkoani Kilimanjaro kusota kwa takribani siku 302 rumande kwa kesi namba 2 ya hujumu uchumi pamoja na utakatishaji wa fedha upande wa Jamhuri umesema upelelezi umekamilika na kuomba tarehe ya karibu kwa ajili ya kufaili vibali.
Akiwa mbele ya Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro, Mwendesha Mashtaka, Sabitina Mcharo amedai upelelezi umekamilika na kuomba mahakama kuwapa tarehe ya karibu kwa ajili ya kuweka vibali pamoja na kuendelea na taratibu nyingine kwa mujibu wa sheria.
"Mheshimiwa upelelezi umekamilika na tunaomba tarehe ya karibu kwa ajili ya kusasilisha nyaraka pamoja na kusikiliza maelezo ya awali," amedai Sabitina.
Upande wa utetezi uliongozwa na Mawakili Hellen Mahuna pamoja na wakili Mosses Mahuna wamefurahishwa na kukamilika kwa upelelezi kutasaidia mteja wao kutambua alipo ikiwa tayari amekaa gerezani zaidi ya siku 302.
"Mheshimiwa kwa upande wa mshtakiwa tumefurahi kusikia upelelezi umekamilika na tunaomba utupatie hairisho fupi ili tuweze kuja tarehe za karibu ili tuweze kuendelea na shauri hilo," amesema Mahuna.
Aidha Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Salome Mshasha ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 5 mwaka huu.
"Kesi hii imeahirishwa hadi Aprili 5 mwaka huu, mshtakiwa tutaendelea kuwa chini ya uangalizi wa magereza na kesi hiyo haina dhamana.
Sabaya mara ya mwisho kufikishwa Mahakama ya Mkazi Moshi ilikuwa ni Desemba 5, 2022 ambapo kesi hiyo ilihairishwa kutokana na hakimu mwenye mamlaka na kesi hiyo kuwa na majukumu mengine ya kikazi.