Vijana Watafuta Soko Kuuza Figo zao Mwanza


Baadhi ya vijana wamedaiwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza kutafuta soko la kuuza figo zao.

Mwanza. Ukistaajabu ya Musa, utaona ya Firauni! Huo ndio usemi unaofaa kuelezea taarifa za baadhi ya vijana kudaiwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza kutafuta soko la kuuza figo zao.


Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu ikiwa ni sehemu ya elimu kwa umma kuhusu afya ya figo, Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Figo Hospitali ya Bugando, Dk Said Kanenda amesema wengi wa vijana hao hutaja hali ngumu kimaisha kuwa miongoni mwa sababu za kufikia uamuzi huo unaokinzana na sheria.


"Tunapata watu wengi, hasa vijana wanakuja wakitaka kuuza figo; wengi wanataja hali ngumu kimaisha kufikia maamuzi hayo. Baadhi wanafikia kutushawishi kwa ahadi ya kupata sehemu ya fedha tikiwawezesha kumpata mnunuzi wa figo zao,” amesema Dk Kanenda.


Ameongeza; "Siyo vijana pekee, bali hata baadhi ya wazee wanakuja kuulizia kama kuna uwezekano wa kuuza figo. Tunawaelimisha kuwa hakuna sehemu duniani pa kuuza figo wala kiungo chochote cha mwili, bali pale panapobidi, viungo hivyo hutolewa kama msaada kwa mgonjwa anayehitaji," amesema.


Bila kutaja takwimu za wanaojitokeza kwa mwaka, Dk Kanenda amesema pamoja na kuwakatalia maombi yao, uongozi wa hospitali hiyo huwatumia wataalam wa saikolojia na masuala ya kiuchumi kuelimisha wahusika namna ya kujipatia kipato kwa njia halali.


“Hakuna biashara ya viungo vya binadamu ikiwemo figo kote duniani; na tunawaeleza ukweli huo vijana na wote wanaojitokeza huku tukiwataka kufanya kazi kwa bidii na ubunifu kujiongeza kipato kuepuka vishawishi vya kuuza viungo vyao,” amesema mtaalam huyo.


 Wagonjwa wa figo

Akizungumzia ukubwa wa tatizo la figo, Dk Kanenda amesema hospitali hiyo inapokea wagonjwa 115 kila wiki wenye matatizo ya figo wanaohitaji huduma ya kusafisha damu kutokana na figo zao kutofanya kazi kwa ufanisi.


“Kila mwezi tunawapokea na kuwahudumia wagonjwa 600 katika kliniki ya figo. Ni vema jamii ijenge utamaduni wa kupima afya kubaini matatizo na kupata tiba mapema kuepuka madhara makubwa,” amesema.


Ametaja mfumo wa maisha ikiwemo watu kutopima afya mara kwa mara kuwa miongoni mwa sababu za ongezeko la wagonjwa wenye matatizo ya figo nchini ambapo asilimia saba ya wakazi wa vijijini wanabainika kuwa na matatizo la figo huku maeneo ya mijini wakiwa ni asilimia 13.


Akizungumzia kitendo cha baadhi ya watu kujitokeza kutafuta soko la viungo vyao vya mwili, Prosper Frank, mkazi wa eneo la Bugarika jijini Mwanza amewataka vijana nchini kuacha tamaa ya mafanikio ya haraka kwa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na maarifa ili kujiingizia kipato halali.


"Kuuza figo siyo ni kinyume cha sheria, bali pia ni kujiweka katika hatari ya kiafya,” amesema Frank.


Kauli hiyo imeungwa mkono na Ashura Songoro aliyewataka vijana kuridhika na vipato vinavyopatikana kwa njia halali badala kutamani mapato ya haraka haraka yanayoweza kuwafikisha kwenye mikono ya sheria

Mwananchi

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad