Wabongo Watamba Mashindano ya CAF


HATUA ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika imebakiza raundi mbili ifike tamati na baada ya hapo timu nane zitatinga robo fainali na nyingine nane zitaaga.

Tanzania inawakilishwa na Simba inayoshika nafasi ya pili kundi C la Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga nafasi ya pili kundi D la Kombe Shirikisho Afrika.

Timu hizo zinahitaji ushindi katika mechi zinazofuata dhidi ya Horoya ya Guinea na Monastir ya Tunisia ambazo zitachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ili zitinge robo fainali.

Wakati Tanzania ikikosa uwakilishi wa angalau refa mmoja katika hatua hiyo, wapo maofisa wanaoshughulika na majukumu mengine ya kisoka wa Tanzania ambao wameitoa kimasomaso nchi kwa kupangwa kufanya kazi tofauti.

Ifuatayo ni orodha ya Watanzania walioula kwa kupewa majukumu tofauti kwenye hatua hiyo.

CLIFFORD NDIMBO

Ofisa habari huyo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) anaongoza kuteuliwa mara nyingi kusimamia masuala ya habari na mawasiliano akiwa amesimamia mechi nne - Simba dhidi ya Raja Casablanca na Simba na Vipers za Ligi ya Mabingwa Afrika na pia za Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe na Yanga dhidi ya Real Bamako.

Pia, Ndimbo atasimamia mechi zinazofuata za raundi ya tano kati ya Simba na Horoya na pia Yanga dhidi ya Monastir mwishoni mwa wiki hii.

KHALID ABDALLAH

Huyu ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya TFF na katika makundi ya mashindano ya klabu Afrika amekuwa akipangwa kuwa kamishna wa mchezo.


Hadi sasa amesimamia michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Zamalek na Esperance na Al Ahly dhidi ya Mamelodi Sundowns.

BARAKA KIZUGUTO

Katika miaka ya hivi karibuni, meneja wa Mashindano wa TFF, Baraka Kizuguto amekuwa akipata fursa ya kusimamia mechi mbalimbali za klabu Afrika katika majukumu ya uratibu wa mechi.


Kama ilivyotegemewa, katika hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu huu, Kizuguto alisimamia mechi ya Mamelodi Sundowns na Al Ahly na pia mechi kati ya Al Merrikh na Zamalek.

JANATHAN KASSANO

Huyu ni meneja wa Ligi wa Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) na ni miongoni mwa maofisa ambao wamekuwa wakifanya vizuri wanapopewa majukumu ya kusimamia mechi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika kwa jukumu la mratibu wa mchezo.

Haishangazi kuona akipangwa kusimamia mechi kati ya DC Motema Pembe na Rivers United kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na pia amepangwa kuwa mratibu wa mchezo kati ya Al Hilal na Mamelodi Sundowns.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad