Kwa namna baadhi ya wanasoka walivyoonyesha vipaji vyao wakati wapo kwenye viwango bora wangekaza buti hadi sasa wangekuwa habari ya mjini ikiwezekana kukipiga nje ya nchi.
Wachezaji hao walipigiwa hesabu na wadau wa soka kuwa wangefika mbali, lakini imekuwa tofauti na matarajio hayo badala yake wamegeuka wa kawaida licha ya wengi wao kujaliwa vipaji vikubwa.
Ni kama wanaendana na kauli aliyowahi kuitoa mwanamuzi mkongwe wa kizazi kipya 20 Parcent kwamba, muziki unampenda ila hapendi muziki kutokana na mashabiki kutamani kumuona akifanya makubwa, lakini ameshindwa kukata kiu yao.
“Nasema hivyo kwani nikitokeza mbele ya watu ama nikipanda jukwaani kuimba nyimbo zangu za zamani zina mwitikio mkubwa. Kutofanya wanachopenda (mashabiki) ndio maana nasema muziki unanipenda ila mimi siupendi, sina maana kuwa sipendi kuimba,” aliwahi kusema 20 Percent.
Tukirejea kwa wanasoka, Mwanaspoti linakuletea baadhi waliopo kwenye gemu na wengine wameendelea na maisha mengine nje ya soka.
EDWARD CHRISTOPHER - NJE
Wakati anapandishwa kutoka Simba B mwaka 2012, Edward Christopher ni kati ya mawinga waliokuwa hatari. Kuna wakati aliwahi kukiri unywaji wa pombe ulichangia kushusha kiwango chake, jambo analojutia na anaamini akipata nafasi nyingine ya kuchezea timu za Ligi Kuu atafanya makubwa.
RAMADHAN SINGANO - NJE
Baada ya kuondoka Azam FC na kwenda TP Mazembe ilikuwa ngumu kumuona winga Ramadhan Singano uwanjani, ingawa anaeleza sababu kubwa ya kukaa nje ni ishu za kimaslahi.
“Ishu yangu haikuwa tofauti na ya Simon Msuva. Sikutaka kuyaweka wazi niliamua kuyamaliza kimyakimya, hivyo msimu ujao nitakuwa uwanjani. Naamini nitakuja na kishindo kingine kwani sijakaa nje kizembe,” anasema Singano ambaye aliibuka katika soka ndani ya Simba ambako aliondoka kwenda Azam baada ya kushindwa kutimiziwa mambo yaliyokuwa kwenye mkataba.
JERRY TEGETE-PAMBA
Wakati yupo Yanga alikuwa anatazamwa kama straika wa nchi kwa namna alivyokuwa anategemewa Taifa Stars, lakini baada ya kuachana na wana Jangwani ni kama ukawa mwisho wa kucheza soka la ushindani. Kwa sasa yupo na Pamba inayoshiriki Ligi ya Championship.
“Kila jambo lina sababu kama wapo wanaoamini nilipotea iwe funzo kwa wanaocheza timu kubwa kulinda viwango vyao na kufika mbali, ingawa naamini nilifanya kwa sehemu yangu na ilikuwa inatosha, wengine hawanifahamu vizuri,” anasema.
MALIM BUSUNGU-NJE
Huyu alikuwa straika wa Yanga na ni kati ya wachezaji walioondoka kwenye gemu mapema na sasa anaendelea na shughuli zake binafsi huku ikielezwa kuwa analima. Lakini endapo angekomaa na changamoto alizowahi kuzitaja kuwa zilimuweka nje kwa sasa angekuwa mbali kwenye soka.
“Kilichoniondoa kwenye soka sikuwa na roho ya uvumilivu. Ninapohitaji haki yangu sipendi dharau jambo linalofanywa na baadhi ya viongozi wa timu. Ndio maana niliamua kukaa pembeni na kuwaachia wengine waendelee na harakati,” aliwahi kukaririwa Busungu ambaye aliichezea pia Mgambo JKT.
GODFREY MWASHIUYA-MBUNI
Yanga ilimsajili kutoka Kimondo ya Mbeya na baadhi ya mashabiki walilinganisha uchezaji wake na staa wa zamani wa timu hiyo, Edbily Lunyamila. Hata hivyo, alishindwa kulinda kiwango, ingawa kwa sasa anacheza Mbuni ya Championship, lakini siyo kwa kiwango kikubwa.
SAID BAHANUZI-NJE
Mwaka 2012 jina lake lilikuwa vinywani mwa mashabiki ndani na nje. Wakati huo alikuwa Yanga ambapo katika Kombe la Kagame alionyesha kipaji na kuibuka kinara wa mabao manane. Ghafla umarufu ukazima na ukawa mwanzo wa kupotea kwenye ramani ya soka. Sndapo angelinda kiwango angekuwa mbali.
Anaelezea kwa nini yupo nje: “Nilikumbwa na changamoto nje ya soka iliyochangia sana kupoteza ramani, ingawa natamani kucheza, lakini sijaonekana muda mrefu ngumu kupata timu.”
SHIZA KICHUYA-NAMUNGO
Kiwango alichoonyesha baada ya kujiunga na Simba 2016 akitokea Mtibwa Sugar kilimpa heshima na kupata ofa mbalimbali kutoka kwa mashabiki, na alikuwa na bahati ya kufunga dhidi ya Yanga katika mechi za watani ambazo zilichangia kumpa umaarufu zaidi.
Kichuya anayecheza Namungo FC kwa sasa, akiwa Simba alipata dili la kujiunga na Pharco ya Misri ambayo ilimtoa kwa mkopo ENPPI ya huko pia. Kama angekaza buti kufikia sasa angekuwa mchezaji ghali zaidi.
IBRAHIM AJIBU-SINGIDA BIG STARS
Kipaji cha Ibrahim Ajibu, kilizifanya Simba na Yanga zihitaji huduma yake, huku wenye jicho la soka wakitamani kumuona akicheza nje na kama angekaza buti angekuwa mchezaji ghali ndani na nje, ingawa bado yupo kwenye gemu, akiitumikia Singida Big Stars.
Licha ya mashabiki kutamani kumuona akifanya makubwa zaidi uwanjani inaonekana ni kama haimsumbui na haonekani kufanyia bidii.
Ajibu aliwahi kulaumiwa na makocha kuwa ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa lakini ana tatizo mazoezi. Nyota wengine ambao wangekaza wangekuwa mbali ni Ibrahim Mohamed , Salum Machaku, Juma Mahadhi, Mohamed Banka, Haji Mwinyi, Joseph Kimwaga, Abdallah Seseme.