Walimu Waghushi Vyeti vya Ndoa Kupata Bima ya Afya

 


Dodoma. Tume ya Utumishi wa Walimu Nchini (TSC), imekabidhiwa majina 78 ya walimu waliobainika kughushi nyaraka mbalimbali za wategemezi na matumizi mabaya ya kadi za bima za afya.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano Serikalini cha TSC iliyotolewa jana Jumatano, Machi Mosi 2023, majina hayo yalikabidhiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).


Walimu hao wanadaiwa kughushi nyaraka za vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya ndoa kwa lengo la kutaka kuthibitisha uhusiano wao na wahusika hao ili waweze kusajiliwa na mfuko huo kwa ajili ya kupata huduma.


Makabidhiano hayo ya majina yamefanyika leo Machi Mosi katika Makao Makuu ya NHIF Jijini Dodoma wakati wa kikao kati ya menejimenti ya NHIF na TSC.


Katika kikao hicho ilitolewa ripoti inayoonesha namna walimu hao walivyohusika katika vitendo vya udanganyifu pamoja na hasara waliyoisababisha kwa mfuko.


Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga amesema mfuko umeshachukua hatua mbalimbali kwa watuhumiwa hao ambao walikiri kutenda makosa hayo.


Amezitaja hatua hizo ni pamoja na kuwafungulia kesi, kuwafungia matumizi ya kadi na kuwataka kurejesha fedha ambazo zilitumika kuhudumia wategemezi wasio halali.


“Tunachukua hatua nyingi kwa watuhumiwa wa udanganyifu na mpaka sasa kuna kesi zinaendelea katika Mikoa ya Geita, Dodoma na Dar es Salaam, kadi za matibabu za watuhumiwa hao zimefungiwa pamoja na kuwaandikia barua za onyo,” amesema.


Naye Katibu wa TSC, Paulina Nkwama amesema kuwa vitendo vilivyofanywa na walimu hao haviwezi kukubalika kwa kuwa ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma hivyo kupitia mamlaka ya tume hiyo hatua zitachukuliwa.


Awali akiwasilisha taarifa ya uchunguzi wa udanganyifu uliofanywa na Watumishi wa Umma, Meneja wa Kitengo cha Kupambana na Udanganyifu cha NHIF, Dk Rose Ntundu amesema watumishi wa umma 99 waliobainika kufanya udanganyifu, 78 ni walimu wa shule za Serikali za msingi na sekondari.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad