Moshi. Mamia ya wanawake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoka bara na visiwani tayari wamefurika katika viunga vya Ukumbi wa Kuringe mjini Moshi, wakimsubiri Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mgeni rasmi kwenye Kongamano la Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Wanawake hao waliingia kwa maandamano ya amani wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwemo yale ya Katiba Mpya.
Maandamano hayo yamefanyika leo asubuhi Machi 8, 2023 kutoka Soko la Kati hadi viwanja vya Ukumbi wa Kuringe yanakofanyika maadhimisho ya wanawake Bawacha kitaifa.
Rais Samia baada ya kumaliza kongamano hilo ataelekea Ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro saa saba mchana na kusalimia wana CCM nje ya ofisi hizo.
Mpaka sasa viongozi mbalimbali wa Chadema wamewasili wakiwemo Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, John Heche, Peter Msigwa, Katibu Mkuu Bawacha, Catherine Ruge, John Mrema pamoja na viongozi wengine wa Kanda na mikoa