Geita. Jeshi la Polisi wilayani Chato mkoani Geita limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waombolezaji na wananchi wa Kata ya Mganza, kufuatia vurugu zilizotokea wakati wa maziko ya kijana Enos Misalaba (32) anayedaiwa kukamatwa na polisi kisha kupigwa na kusababisha kifo chake.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale amethibitisha kutokea tukio hilo na kusema yupo njiani kuelekea eneo la tukio na taarifa zaidi atazitoa baada ya kufika Mganza.
Kaka wa marehemu, Samweli Misalaba akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, amesema wakiwa kwenye eneo la maziko kwa taratibu za mazishi, wananchi walikataa kuendelea na maziko baada ya msomaji risala ya marehemu kusema amekufa kwa ugonjwa wa kifua na siYo kupigwa kama jamii inavyoamini.
“Tulikubali kuzika, tumeshachimba kaburi wakati wa historia ya marehemu msomaji alisoma kuwa amekufa kwa kuugua kifua ndio wananchi wakakataa na kubeba jeneza na kuurudisha mwili kituoni wakitaka waelezwe kifo cha marehemu kimetokana na nini. Wakarudisha mwili kituoni polisi, wakaanza kupiga mabomu ya machozi na wananchi wakaendelea kuandamana,” amesema ndugu wa marehemu.
Enos Misalaba anadaiwa kukamatwa siku ya Jumatatu Machi 27 akituhumiwa kuiba betri ya gari na alikamatwa na polisi wa Kituo cha Mganza. Inadaiwa alipigwa na kuzidiwa kisha kupelekwa kwenye Kituo cha Afya Mganza na Jumanne asubuhi alipoteza maisha akipatiwa matibabu.