Takribani watu 60 wamepata huduma ya kuwekea puto tumboni ili kupunguza uzito katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Mohamed Janabi ambapo amesema kuwa kati ya watu hao, ni mtu mmoja tu lilimshinda, akatolewa na kwamba hilo ni jambo la kawaida.
“Kuwepo kwa huduma ya kupunguza uzito na kupunguza mafuta mwilini ni sehemu ya utalii wa matibabu hivyo tunatarajia kupata watu wengi zaidi,” alisema.
Profesa Janabi ameeleza kuwa utoaji huduma hiyo unahusisha uingizaji wa mrija wa puto kupitia mdomoni, hali itakayopunguza kiwango cha chakula kwa mhusika.
“Tutaweka kwa miezi nane, tutaingiza kupitia mdomoni hadi kwenye tumbo hakuna upasuaji, tutatumia mitambo ifike mahali pake tutajaza dawa linapunguza ukubwa wa tumbo, ukila kidogo utashiba hivyo tunategemea uzito utapungua,” amesema Janabi
Aidha amefafanua gharama ya huduma hiyo nje ya nchi inategemea na nchi na kwamba, India ni Sh milioni 15 hadi 20 na Ulaya milioni 30 kwenda juu lakini hapa nchini ni Sh milioni 4 hadi milioni 4.2.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, Profesa Mohamed Janabi
“Ni tiba salama kama tunavyopandikiza figo, uloto na zingine wakitaka kupata huduma hapa ni rahisi,” amesema.
Profesa Janabi alieleza kuwa faida kubwa ni kusaidia kukukinga na magonjwa ya kisukari, kiharusi, moyo, kushindwa kupumua.
“Siku ya kwanza unaweza kusikia kama una vidonda vya tumbo lakini baada ya muda utaendelea kawaida, hospitali hatukaribishi watu lakini tunawaomba wale wenye uzito mkubwa wafike kliniki, tuna kliniki ya siku mbili hapa Mloganzila na siku mbili Muhimbili Upanga,”amesema .
Pamoja na hayo alisema pindi mgonjwa anapopatiwa huduma hiyo na kupungua atapata usaidizi wa mtaalamu wa lishe ili asiongeze tena kiwango cha kula na uzito kuongezeka tena.
“matatizo mengine ni ya kurithi, ukiwa na mtoto ana uzito mkubwa mleteni, wakati mwingine unaweza kukuta mtoto amezaliwa na kilo nne watu wakaona ni kitu sahihi kumbe sio kweli.”