Mkurugenzi wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania imetangaza kuchukua hatua kali za kisheria kwa chombo chochote cha utangazaji ambacho kitabainika kuendeela kurusha taarifa zenye maudhui ya kufikirika kuhusu imani za kidini.
Pia imeonya kwamba taarifa zozote za masuala ya dini zinazotolewa kwa umma kupitia vyombo vya utangazaji zinatakiwa kuwa za kweli, uhakika na zitoke katika vyanzo vinavyoaminika ili kuepusha upotoshaji kwa jamii.
Onyo hilo limekuja siku chache baada Mhubiri Diana Bundala maarufu kama ‘Mfalme Zumaridi’ kuibua mijadala kuhusu taarifa za kufikirika alizozitoa kuhusu masuala ya imani ya kidini pindi alipohojiwa na chombo kimoja cha habari.
Kutokana na hali, Mkurugenzi wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari Machi 21, 2023 amekemea vikali hali hii ya taarifa za mawazo ya kufikirika na yenye utata kuhusu imani za kidini.
Amesema taarifa hizo zinaendelea kushamiri kwenye vyombo vya utangazaji vya mitandao na vile vya redio na runinga za kawaida hivyo kuagiza kuacha mara moja kurusha maudhui yoyote ya kufikirika ambayo yanaleta utata kuhusu imani za kidini kwenye jamii.
“Siku za hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa taarifa fupi zilizo kwenye mfumo wa video clip zinazozungumzia masuala yanayohusu mawazo, fikra yanayogusa imani za kidini. Mawazo hayo yamekuwa yakitolewa kwenye vyombo mbalimbali vya utangazaji ikiwa ni pamoja na Radio na Televisheni, vyombo vya utangazaji mitandaoni na kwenye makundi ya mitandao ya kijamii.
“Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapenda kuchukua nafasi hii kutoa ufafanuzi kwamba masuala kama hayo yanayohusu imani za dini ni masuala binafsi ya mtu na hivyo mahali sahihi ni kwenye nyumba za ibada na sio kwenye vyombo vya habari na utangazaji,” amesema.
Amesema vyombo vya habari na utangazaji vina wajibu wa kufuata misingi na maadili ya taaluma zao kwa kutoa taarifa zilizofanyiwa uchambuzi na kuaminika na za kweli hii ni pamoja na kutoa taarifa kwa kufuata sheria, kanuni, miongozo na maadili katika kutoa huduma ya utangazaji nchini.
Amesema kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta (maudhui ya utangazaji wa redio na televisheni) za mwaka 2016 na kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta maudhui ya utangazaji mtandao ya mwaka 2022, zimeelekeza watoa huduma ya utangazaji kujiepusha na maudhui ya upotoshaji na yanayogusa imani za watu.
“Hivyo basi, taarifa zozote zinazotolewa kwa umma kupitia vyombo vya utangaza ziwe za kweli, uhakika na zitoke katika vyanzo vinavyoaminika ili kuepusha upotoshaji kwa jamii,” amesema.