Kenya. Mwanamume anayekadiriwa kuwa na miaka 43, amefariki dunia juzi usiku Jumamosi katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi nchini Kenya, huku akiwa ameshika mkononi begi lake kwenye eneo la kusubiri wasafiri uwanjani hapo.
Abiria huyo ambaye jina lake hakufahamika mara moja, inaelezwa alikuwa akisubiri ndege ya kwenda jijini Mombasa.
Chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika, huku tukio hilo likiacha mshangao kwa abiria walikuwa eneo hilo.
Polisi nchini humo wanaendelea na uchunguzi zaidi kutokana na kifo cha abiria huyo.
Kwa mujibu wa polisi, mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 43 alikuwa akielea Mombasa usiku wa Jumamosi Aprili 8,2023.
Pia alikuwa amemaliza taratibu zote uwanjani hapo, lakini ikashindikana kuendelea na safari baada ya kubainika alikuwa ameshafariki dunia akiwa kwenye kiti.
“Wahudumu wa Shirika la Ndege la Jambojet walimwita jina lake mara kadhaa hata hivyo hakuitika,” ameeleza mmoja wa shuhuda wa tukio hilo
Taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa Tuko wa nchini humo imeeleza kwamba, maafisa wa uwanja wa ndege wamesema mwanamume huyo alikuwa amekaa kwenye kiti katika eneo la kusubiri abiria wanaosafiri na aliaga dunia huku akiwa ameshika begi lake mkononi.
Baada ya kubainika kuwa kulikuwa na tatizo kutokana na kutoamka wala kuitika, wahudumu wa afya katika uwanja wa ndege waliitwa na kubaini kuwa alikuwa ameaga dunia.
Baada ya tukio hilo, polisi waliitaarifu familia ya marehemu, huku wakiahidi kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
Hata hivyo, mwili wake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi ya maiti ambako uchunguzi zaidi wa polisi utafanyika.