Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema kama kuna msanii ambaye hajaridhishwa na mchakato wa tuzo za Tanzania (TMA) basi afike BASATA na ataoneshwa hatua zote za upembuzi zilizomtoa katika mchakato wa tuzo.
Akizungumza na TBC mratibu wa tuzo za TMA, Mrisho Mrisho kutoka BASATA wakati akijibu malalamiko ya msanii Mbosso ambaye hivi karibuni aliandika katika ukurasa wake wa Instagram akishangaa kwanini EP yake ya ‘Khan EP’ haijaingizwa kwenye EP bora ya mwaka, amesema unapoweka albamu unaichia jopo lifanye tathmini na yenyewe ndiyo itakayotoa maamuzi.
“Maamuzi hayo sasa si ya Mbosso kusema kwamba mimi EP yangu ni bora kuliko..,hapana usidharau kazi ya wengine, wasanii wote wanafanya kazi," amesema.
Hata hivyo Mrisho amemkaribisha msanii huyo kufika katika ofisi za BASATA ili kufunguliwa akaunti na kuoneshwa mfumo mzima wa mchakato wa tuzo hizo.
.