Bei mpya ya mafuta yazidi kushuka



Dar es Salaam. Italeta ahueni ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) leo kutangaza bei mpya za ukomo wa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji na thamani ya shilingi ikilinganisha na dola ya Marekani.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Aprili 4,2023 na Mkurungenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule imeeleza kuwa bei hizo zitaanza kutumika kuanzia Jumatano Aprili 5 mwaka huu.

Kwa mujibu wa viwango vipya vya bei vilivyotangaza na Mamlaka ya Udhiti wa Nishati na Maji (Ewura) jana bei ya dizeli imepungua kwa Sh28, petroli Sh187 na mafuta ya taa kwa Sh169 kwa lita, ukilinganisha na bei za mwezi uliopita.


Kwa viwango hivyo vipya Jiji la Dar es Salam bei ya petroli itakuwa Sh2,781 kwa lita, dizeli Sh2, 847 na mafuta ya taa Sh2,929 na bei ya juu zaidi itakuwa katika Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ambapo petroli itauzwa Sh3,019, dizeli Sh3,084 na mafuta ya taa Sh3,167.

“Kwa mikoa ya Kaskazini Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, bei za rejareja za Aprili mafuta ya petroli imepungua kwa Sh158, dizeli Sh158 na mafuta ya taa Sh231, ikilinganishwa na toleo la Machi Mosi mwaka huu,” imeleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na kuisha kwa mafuta ya taa kwenye matanki ya kuhifadhia yaliyopo Tanga, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka katika bandari ya Dar es Salaam.

“Bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika,”

Kwa Mikoa ya Kusini Mtwara, Lindi, na Ruvuma, bei za rejareja za Aprili 2023 kwa mafuta ya petroli imepungua kwa Sh220, dizeli Sh220 na mafuta ya taa Sh176 iwa lita ikilinganishwa na toleo la Machi Mosi.

 “Kwa kuwa hakuna matanki ya kuhifadhia mafuta ya taa katika Bandari ya Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kusini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa,”

Katika taatrifa hiyo Dk Mwainyekule alibainisha kuwa tofauti ya bei kutoka sehemu moja kwenda nyingine inatokana na tofauti ya bandari mafuta yanapochukuliwa na gharama ya usafirishaji.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad