Baada ya Mahakama kuu ya Tanzania, masijala kuu DSM kumtaka Cyrpian Musiba kumlipa Mhe.Bernard Membe TZS 9.9 Bilioni, kwa kumchafua kupitia magazeti yake, Kampuni ya Yono Auction Mart imepewa Idhini Kupiga Mnada Mali zote za Musiba Ili Kumlipa Membe Fidia inayohitajika.
Kufuatia hali hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho nchini, Emmaus Mwamakula alimuandikia barua Membe kumuomba amsamehe Musiba kwa kuwa hana uwezo wa kulipa Biliini 9 na pia ameshasalimu amri.
Leo Membe amemjibu Askofu Mwamakula kama ifuatavyo;
________________
Baba Askofu Salaam,
Asante kwa barua yako ambayo umenitaka nimsamehe Musiba kwa sababu amesalimu Amri na kwamba hana hela ya kunilipa hata kama atauza kijiji.
Baba Askofu, sababu ulizozitoa hazina mashiko kwa sababu Musiba hajaniomba radhi, hajasalimu amri popote, na hata kama amesalimu, basi amechelewa! Aidha hata kama hana hela kama unavyosema, anazo mali zisizohamishika na hizo zote zitapigwa mnada.
Musiba anajua kuwa siwezi kumsamehe kwa sababu nilimpatia nafasi tatu za wazi za kuomba radhi kwenye Chama akapuuza. Nilimpatia nafasi ya kuomba radhi kwenye magazeti yake akapuuza. Na kabla ya kesi haijaanza nilimpatia muda wa kulimaliza jambo hili nje ya mahakama, lakini nafasi zote hizo alizikataa.
Kwahiyo, Sitamsamehe kamwe na anastahili adhabu hiyo ili awe na adabu na iwe fundisho kwa wengine wenye tabia za kijinga kama hizo.
Nawashukuru Majaji wote wa mahakama kuu kwa uvumilivu na kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kunirudishia heshima yangu na kuuthibitishia umma kuwa katika nchi hii kuna uhuru wa Mahakama na uongozi unaoheshimu sheria. Vinginevyo nakushukuru kwa barua na mawazo yako! Ubarikiwe.!
Bernard Camiluus Membe,
Waziri na Mbunge mstaafu.!