FUNDI wa mpira kutoka Zambia anayekipiga Simba SC, Clatous Chama amebakisha mabao mawili pekee ili kumfikia nyota wa Tanzania na klabu ya Genk, Mbwana Samatta.
Baada ya kufunga mabao matatu katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Horoya, Chama alifikisha mabao manne na kuwa kinara wa mabao katika msimamo wa wafungaji, mabao hayo yamemfanya kufikisha jumla ya mabao 19 katika historia ya Ligi ya Mabingwa.
Samatta aliwahi kucheza TP Mazembe na msimu wa 2015 akatwaa ubingwa wa Afrika akiwa na timu hiyo, katika kipindi chote alichocheza michuano hiyo Samatta alifunga mabao 21, hata hivyo msimu huo alitwaa tuzo ya ufungaji bora.
Mabao 19 ya Chama yanamfanya kuingia katika orodha ya wafungaji 10 bora wa muda wote katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu yalipoanzishwa 1964 .
Kati ya mabao hayo,15 amefunga akiwa na Simba mabao manne amefunga akiwa na Zesco United ya Zambia, ambapo kwa msimu huu tayari amefunga magoli matano pamoja na lile la Premeiro De Agosto.
Wachezaji wanaoongoza kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote namba moja ni Tresor Mputu akiwa na mabao 39, nafasi ya pili ni Mohamed Aboutrika 31, Mahmoud El Khatib, 28, Flavio Amando 27, Emad Moteab 24, Ali Zitouni 23, Mbwana Samatta 21, Dioko Kaluyituka na Mouhcine Iajour 20, Clatous Chama 19, Gamal Abdel-Hamid, Kelechi Osunwa na Mudather El Tahir, 18.
Simba imeingia kwenye hatua ya robo fainali endapo Chama atafunga mabao mawili atakuwa amemfikia Mbwana Samatta.