Wakati ilipotangazwa mastaa kibao wa Simba, Yanga na Azam wameitwa katika timu zao za taifa, kijiweni kulikuwa na shangwe la kufa mtu kila upande ukijisifia kuwa umejaza mastaa ambao wanatambulika kwenye mataifa yao.
Kilichotokea kwa mastaa hao katika mechi za timu zao za taifa za kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyika Ivory Coast kilikuwa tofauti na matarajio ya wengi. Kuna kitu cha kujifunza.
Mastaa wetu wengi walisotea benchi kwenye timu zao za taifa na wale waliocheza ilikuwa kwa dakika chache sana na wengi waliingia wakati mpira unakaribia kumalizika.
Ninaowazungumzia hapa ni Clatous Chama ambaye anaongoza kwa kupiga pasi za mwisho katika Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele ambaye ni mfungaji anayeongoza kwenye ligi msimu huu, Saido Ntibazonkiza aliyehusika na idadi kubwa ya mabao lakini wapo kina Stephane Aziz Ki, Djigui Diarra, Henock Inonga, Kennedy Musonda, Peter Banda na wengineo.
Kukaa kwao nje kukafanya baadhi ya watu hapa kijiweni waseme kuwa ligi yetu sio imara ndio maana mastaa wetu wameshindwa kucheza katika timu zao za taifa lakini kiuhalisia hawakuwa sahihi na ni kama waliwaonea.
Tatizo halikuwa kwamba ligi yetu sio bora, bali ambao walicheza nafasi zao ni wachezaji wanaocheza ligi kubwa zaidi duniani na wenye uwezo mkubwa kuliko hao mastaa wetu.
Kikosi cha DR Congo, washambuliaji wawili waliomuweka nje Mayele, mmoja ni Cedrick Bakambu ambaye anachezea Olympiacos ya Ugiriki aliyoifungia mabao 13 na kupiga pasi za mwisho tatu katika mechi 22 msimu huu.
Ukiondoa Bakambu, kuna Gael Kakuta wa Lille ya Ufaransa ambaye kafunga mabao matatu katika mechi 16 za timu hiyo msimu huu.
Ukija kwa Chama, viungo watatu wanaomuweka benchi Zambia kuna Emmanuel Banda anayecheza Rijeka ya Croatia, Benson Sakala wa Pribram ya Czech na Kings Kangwa wa Red Star Belgrade ya Serbia.
Ukipata muda wako, angalia wasifu wa wachezaji walioanza katika nafasi za kina Banda, Aziz Ki, Diarra, Musonda, Sakho na Inonga utakubaliana nami kwamba ilikuwa lazima kusotea benchi.
Tunawapenda mastaa wetu lakini kwao kuna wajanja zaidi yao.