Dar es Salaam. Unalikumbuka tukio la basi la mwendokasi lililoacha njia na kugonga ukuta wa jengo lililopo Kisutu jijini Dar es Salaam huku likimkosa mwenda kwa miguu aliyekuwa akikatisha mtaani hapo? Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) imesema anastahili kulipwa fidia.
Wakati Tira ikisema hivyo, familia ya Osam Milanzi aliyenusurika katika ajali hiyo ya Februari 22, inapitia sintofahamu ya kumtibu ndugu yao.
Hata hivyo, Esha Mohammed, mke wa Osam hafahamu chochote kuhusu fidia hiyo, akidai mawasiliano yao na mabosi wa mwendokasi yalikatika tangu mumewe aliporuhusiwa kutoka hospitalini.
“Tangu ametoka hospitali hatuna msaada wowote, wale waliomsababishia ajali tumeambiwa walipaswa kugharimia malipo ya hospitali tu, aliporuhusiwa kurudi nyumbani hakuna kingine tunachokifahamu kutoka kwao. Aprili 4 anapaswa kurudi kliniki, anahitaji kupata wheelchair, dawa, magongo na hata lishe, maisha yetu tulimtegemea yeye hivyo tunasubiri kudra za Mwenyezi Mungu tu,” alisema Esha.
Anasema mumewe bado ana maumivu ya mkono wa kulia na mguu wa kushoto ambao alifanyiwa upasuaji na kuwekewa vyuma.
“Hata upasuaji ulichelewa baada ya kutakiwa kulipa Sh600,000 ambazo familia hatukuwa nazo na wale waliomsababishia ajali walizitoa kwa kuchelewa,” alisema.
Nyumbani kwa Osam, Manzese Midizini, watu wakiwamo majirani, ndugu, jamaa na marafiki hawakauki kumjulia hali, ingawa mkewe anasema huwa anaangua kilio kumbukumbu zinapomrudia na kuwatambua waliomtembelea.
“Baada ya ajali, amepata tatizo la kupoteza kumbukumbu, unaweza kumuuliza kitu, anapoanza kukujibu anabadilisha na kuzungumza kitu kingine,” anasema Esha na ndicho kilitokea hata alipozungumza na gazeti hili juzi Alhamisi nyumbani kwake, katikati ya mazungumzo yalibadilika na kuanza kuomba radhi akieleza ni kwa sababu hakutekeleza ahadi yake ya jana.
Mkewe alilazimika kumkatisha kwa kumtikisa na kumuita jina lake, ndipo anarudi kwenye mazungumzo ya kawaida.
“Hii ndiyo changamoto yake, ni baada ya kuumia kichwani katika ajali ile japo daktari aliniambia atakuwa sawa na katika vitu ambavyo amesema tusimuulize ni kuhusu ajali, kwani inaweza kumrudisha kwenye kumbukumbu mbaya zaidi na kumsababishia tatizo jingine,” alisema.
Tangu kutokea kwa ajali ile, alisema Osam hafahamu wala hakumbuki kama aligongwa na basi ila anajua kwamba anaumwa.
“Hata tulipokuwa hospitali, kuna muda alikuwa akiniuliza ni kwa nini yuko pale, anachokifahamu ni mgonjwa, ila nini kimesababisha yeye kuwa kitandani hafahamu hadi sasa,” alisema.
Kwa hali aliyonayo mumewe, anasema hawezi kufanya kitu chochote kwa sasa hata kunyanyuka na kufanya mazoezi ni kwa msaada wa magongo ambayo alisaidiwa na jirani yao mmoja japo si ya saizi yake ila wanayatumia hivyohivyo.
“Hawezi kupanda daladala, inapofika siku ya kwenda kliniki, lazima tujue anafikaje. Mguu alifanyiwa upasuaji na kuwekewa vyuma, japo ulichelewa kutokana na pesa iliyohitajika kupatikana kwa kuchelewa, watoto wanahitaji kwenda shuleni, nauli, chakula na mahitaji mengine kama baba alikuwa akiyafanya yeye, sasa hana uwezo huo,” alisema Esha, mama wa watoto watatu.
Esha ambaye ni mama wa nyumbani anasema mwanzoni baadhi ya wasamaria wema waliwasaidia na kupata ahueni ya maisha.
“Kwa sasa hatuna kitu, kula yetu ni ya siku hiyohiyo tunachokipata, kikiisha basi hatufahamu kesho itakuwaje. Osam ndiye alikuwa kila kitu kwetu, sasa ni mgonjwa hawezi kufanya chochote, kila kitu anahitaji kusaidiwa kutokana na hali yake,” alisema Esha.
Kwa hali aliyonayo mumewe, Esha anaomba msaada wa wasamaria. Ili kumsaidia Osam, unaweza kuwasiliana na mkewe kwa namba 0748 152 830 iliyosajiliwa kwa jina la Esha Mohammed Issa.
Esha anayemwelezea mumewe kuwa alikuwa mtu wa kuswali sana, anasema siku ya tukio kama kawaida yake aliamka kuwahi swala ya asubuhi.
“Huwa anapenda kufanya mazoezi, alifanya hapa nyumbani, akajiandaa na akaniaga anakwenda msikitini kisha ataelekea kibaruani.
Tira, Udart wanena
Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Tira, Phostine Oyuke alisema fidia zipo na anachopaswa kufanya Osam ni kuripoti kwenye kampuni ya bima.
“Awe na bili ya hospitali, na lazima awe na taarifa ya polisi ya pande zote mbili, katika fidia za bima, atalipwa gharama za matibabu hospitalini, gharama za usafiri na kama ni mfanyakazi anaingiza kipato kila siku kwa siku ambazo ameshindwa kufanya kazi, fidia inakuwepo pia,” alisema Oyuke.
Mkurugenzi wa kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), John Nguya alisema mabasi yao yote yana bima hivyo kila kitu kitagharimiwa.
“Wakishamaliza kufuata taratibu na mgonjwa amepona, wanapeleka nyaraka zinazohitajika zitakaguliwa basi taratibu nyingine zitaendelea. Toka siku ya kwanza tumewaelimisha, tuliwapelekea watu wakazungumza na mgonjwa na kuwaeleza wakishatoka hapo nini wafuate, hakuna siri kwenye hili, ni kitendo cha kukamilisha taratibu za bima tu,” alisema Nguya.