Hatimaye Simba Wafanikiwa Kufuta Uteja Kwa Yanga...Yamchapa 2 Bila


Dar es Salaam. Mchezo wa 'Kariakoo Derby' kati ya Simba na Yanga umemalizika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji kushinda mabao 2-0 na kufuta uteja wa siku 1520.

Mabao ya Simba yamefungwa na beki, Henock Inonga dakika ya pili ya mchezo huku Kibu Denis akifunga la pili kwa shuti kali lililomshinda kipa Diarra dakika ya 32.

Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huo,

Huu ni mchezo wa 110 baina ya timu hizi kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965 ambapo kati ya hiyo Yanga imeshinda 38 huku Simba ikishinda 32 na mechi 40 zikiisha kwa sare.

Katika michezo hiyo 110 safu ya ushambuliaji ya Yanga ndio ambayo imekuwa tishio tofauti na kwa wapinzani wao kwa sababu imefunga jumla ya mabao 113 huku kwa Simba ikifunga 103.

Mabao tisa (9) kati ya 14 yaliyofungwa katika mechi 11 zilizopita za Ligi Kuu Bara baina ya timu hizi yamewekwa kimiani na wachezaji wa kigeni huku matano tu yakifungwa na wazawa.

Katika michezo 11 iliyopita ya Ligi Kuu Bara kati ya timu hizo, Yanga imeibuka na ushindi mara mbili huku Simba ikishinda mara tatu wakati michezo sita iliyobakia ikimalizika kwa sare.

Katika michezo hiyo safu ya ushambuliaji ya Simba imefunga jumla ya mabao manane huku Yanga ikifunga sita.


Simba imevunja uteja wa siku 1520 kwa kuifunga Yanga katika Ligi Kuu Bara tangu mara ya mwisho iliposhinda bao 1-0, Februari 16, 2019, lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere anayeichezea Singida Big Stars.

Tangu mwaka 1965, timu hizi zimekutana mara 13 kwa mwezi huu wa Aprili ambapo Simba imeshinda minne huku Yanga ikishinda mitatu wakati sita iliyobakia ikimalizika kwa sare.

Katika michezo hiyo safu ya ushambuliaji ya Simba imefunga jumla ya mabao 15 huku Yanga ikifunga 14.


Huu ni mchezo wa 36 kwa timu hizi kukutana katika Ligi Kuu Bara kwa siku ya Jumapili tangu mwaka 1965 ambapo Simba imeshinda 10 na kupoteza saba huku 19 ikimalizika kwa sare.

Hata hivyo kwa Yanga ndio timu ya kwanza kushinda mchezo uliochezwa siku ya Jumapili baada ya kuifunga Simba bao 1-0, Juni 18, mwaka 1972, lililofungwa na Leonard Chitete.

Katika michezo hiyo 36 Simba ndio timu pekee ambayo imekuwa mwenyeji mara nyingi zaidi (mechi 21) huku Yanga ikiwa mwenyeji mara 15.

Mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa timu hizi kukutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ilikuwa ni Oktoba 26, 2008 ambapo Yanga ilishinda bao 1-0, lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Ben Mwalala dakika ya 15 tu.

Kocha Mkuu na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni ndiye anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao matatu 'Hat-Trick' katika mchezo wa 'Derby ya Kariakoo' uliopigwa Julai 19, 1977.

Katika mchezo huo Simba ilishinda mabao 6-0 huku mbali na Kibadeni aliyefunga matatu, ila wengine ni Jumanne Hassan 'Masimenti' aliyefunga mawili wakati Selemani Sanga akijifunga mwenyewe kwa upande wa Yanga.

Tangu mara ya mwisho Yanga ifungwe mabao 2-1 na Ihefu katika Ligi Kuu Bara Novemba 29, mwaka jana, huu ni mchezo wa 13 ambapo kati ya hiyo imeshinda 12 na kupoteza mmoja tu.

Katika michezo hiyo 13, safu ya ushambuliaji ya Yanga imefunga jumla ya mabao 26 na kuruhusu matano tu.

Huu ni mchezo wa saba katika Ligi Kuu Bara kwa Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' kuiongoza timu hiyo tangu alipotangazwa rasmi Januari 3, mwaka huu akichukua nafasi ya Juma Mgunda ambaye ni msaidizi wake.

Katika michezo hiyo ya Robertinho ameshinda sita na kutoka sare mmoja tu ambao ni wa bao 1-1 na Azam FC uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Februari 21, mwaka huu ambapo safu ya ushambuliaji ya timu hiyo imefunga mabao 15 na kuruhusu manne tu.

Mchezo wa mwisho baina ya timu hizi uliopigwa Oktoba 23, mwaka jana zilifungana bao 1-1 ambapo Simba ilitangulia kupitia kwa Augustine Okrah dakika ya 15 kisha Stephane Aziz KI akaisawazishia Yanga dakika ya 45.

Katika michezo 26 ambayo Simba imecheza imeshinda 19, sare sita na kupoteza mmoja tu ikiendelea kusalia nafasi ya pili na pointi zake 63.

Kwa upande wa Yanga katika michezo 26 pia iliyocheza imeshinda 22, sare miwili na kupoteza miwili ikiendelea kusalia kileleni na pointi 68.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad