Kocha wa Simba Afunguka Kuelekea Mechi yao na Waydad "Hawataamimi Macho yao"



HUKU Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira akisema kikosi chake kiko tayari kwa ajili ya mechi ya mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali itakayochezwa kesho saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa Mohamed wa Tano dhidi ya Mabingwa Watetezi

Wydad Athletic Club nchini Morocco, kiungo 'tindo' wa timu hiyo, Mzamiru Yassin, amesema wao kama wachezaji wanaitaka sana mechi hiyo.

Akizungumza akiwa nchini humo, kocha huyo, amesema mbele ya wanahabari kuwa wachezaji wake hawana hofu na mechi hiyo kutokana na kwamba wengi wao ni wazoefu wa michuano ya kimataifa na wameshacheza mechi nyingi ugenini.

Robertinho alisema kwenye mechi ya kesho anachoamini ni mbinu zake ambazo amezitengeneza kwa wachezaji kuelekea mechi hiyo ingawa hakutaka kuzitaja hadharani, akiweka wazi kwamba zitaonekana uwanjani na kuwashangaza wapinzani wao.

"Ni mechi ngumu, tunacheza na mabingwa watetezi, lakini tunaamini kwenye mbinu zetu tulizokuja nazo, sitozitaja hapa, haitokuwa mechi rahisi, lakini nina kundi la wachezaji ambao ni wazoefu wa kucheza mechi na timu kubwa tena ugenini, na pia haitokuwa mara ya kwanza kuja kucheza hapa, tulishawahi kuwapo hapa kucheza na Raja Casablanca kwa hiyo wachezaji wangu wameshazoea mazingira ya hapa, utakuwa mchezo mzuri na mgumu pia," alisema Robertinho.


Hata hivyo, licha ya baadhi ya wadau wa soka nchini kuikatia tamaa Simba kushinda ugenini dhidi ya Wydad, Mzamiru amesema hawana muda wa kusikiliza mengi yanaowakatisha tamaa kuelekea mchezo huo wa marudiano na badala yake imani yao ni moja tu 'inawezekana'.

Simba imewasili juzi usiku mjini Casablanca tayari kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano dhidi ya wenyeji wao, Wydad ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 walioupata Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita na Mzamiru anasema umewaaminisha inawezekana na wanaamini watafikia lengo lao la kutinga hatua ya nusu fainali wanayoisaka zaidi ya miaka minne kwa sababu wachezaji wote wanaari na wanautaka vilivyo mchezo huo.

Alisema anatambua mchezo huo utakuwa mgumu na ushindani mkubwa kwa sababu wanahitaji kuendeleza ushindi walioupata nyumbani na kuhakikisha wanaulinda katika mchezo huo wa marudiano.


“Tutaenda uwanjani tukiwa na akiba ya ushindi wa nyumbani na kitendo cha kumfunga bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ni rekodi kubwa kwetu na inatupa nguvu ya kuamini inawezekana.

"Tumeifunga timu kubwa nikiwa miongoni mwa wachezaji waliocheza dakika 90, ni rekodi kubwa kwetu bado tuna dakika nyingine 90 ngumu kuhakikisha tunatinga hatua inayofuata,” alisema Mzamiru ambaye ametokea kuwa kipenzi kikubwa cha mashabiki wa timu hiyo.

Aliongeza kuwa maneno mengi yanayozungumzwa hawayapi nafasi, wanachokiangalia sasa ni namna watakavyojiandaa kuwakabili Wydad kwa dakika 90 ngumu kwao.

“Wachezaji tunautaka sana huu mchezo, na malengo yetu ni kucheza nusu fainali, tuna waheshimu wapinzani wetu na tutacheza kwa nidhamu kubwa ili kutafuta ushindi ugenini jambo ambalo linawezekana,” alisema kiungo huyo.

Naye aliyekuwa Kocha wa Simba na sasa akiinoa KCCA FC ya Uganda, Jackson Mayanja, aliliambia gazeti hili jana kuwa anaimani na timu yake hiyo ya zamani kufanya vizuri katika mchezo huo wa marudiano dhidi ya Wydad.

Alisema anafahamu uwezo wa Robertinho na kwamba kama wachezaji wake wakijitoa kwa jasho katika mchezo huo watafanya vizuri.

“Tunatakiwa kuheshimu dakika 90 ambazo zitakuwa za timu zote mbili kwa Simba na Wydad Casablanca, tusiwakatie tamaa Simba, mpira ni mchezo wa kikatili na lolote linaweza kutokea kwa wawakilishi hao wa Afrika Mashariki na Kati waliobaki katika Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Mayanja.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad