KOCHA Mkuu wa Simba, Jumatatu wiki hii alifanya uammuzi mgumu wa kuwapumzisha kwa makusudi nyota wake muhimu wawili tegemeo ili kucheza dhidi ya Yanga, Jumapili hii.
Wachezaji hao walikosekana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu uliopigwa Jumatatu ya wiki hii kwenye Uwanja wa Highland uliopo Mbarali jijini Mbeya ambapo Simba ilishinda 0-2, mabao yote yakifungwa na Jean Baleke.
Nyota hao wawili waliopumzishwa ni kiungo Clatous Chama na Mohamed Hussein ambaye ni nahodha msaidizi wa kikosi hicho.
Mmoja wa Mabosi wa Benchi la Ufundi la Simba, ameliambia Spoti Xtra kuwa, Chama aliachwa Dar kutokana na kuhofia kupata majeraha.
Aliongeza kuwa, mchezaji mwingine aliyepumzishwa kwa makusudi ni Hussein Mohammed ‘Tshabalala’ ambaye yeye alisafiri na timu, lakini baada ya uongozi kugundua ana kadi mbili za njano, wakamtoa kwenye mpango wa kucheza.
“Chama ndiye mchezaji aliyetumika sana katika timu akiwa amecheza michezo mingi katika michuano tunayoshiriki msimu huu ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara.
“Hivyo ilikuwa lazima apumzishwe kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Kariakoo Dabi, hivyo benchi la ufundi kwa pamoja likakubaliana kumbakisha Dar.
“Pia Tshabalala aliondolewa kikosini katika hatua za mwisho wakati kikosi kinapangwa, hiyo ni baada ya kugundua ana kadi mbili za njano, hivyo uongozi ukakubaliana kumuondoa kwa hofu ya kupata kadi nyingine ambayo ingemfanya aiokose Kariakoo Dabi,” alisema bosi huyo.
Alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally kuzungumzia hilo, alisema: “Hilo ni suala la kiufundi, hivyo ngumu kwangu kuzungumzia, lakini ni kweli Chama hakuwa katika msafara wa timu, alibakishwa Dar.”