Kuelekea mchezo wa kesho wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF, Kocha mkuu wa Yanga SC, Nasredinne Nabi na nyota Benard Morisson wamezungumza na waandishi wa habari hapa Nigeria.
Yanga SC itashuka dimbani kesho saa 10:00 jioni kwa saa za Tanzania kucheza na wenyeji wao Rivers United.
“Hongera kwa uwanja mzuri. Niwapongeze pia uongozi wa Yanga kwa kuhakikisha tumekuja mapema hapa Nigeria. Hali ya hewa ni nzuri na tumekuwa na maandalizi mazuri”, alisema kocha Nabi.
“Hatujioni wakubwa kwa sababu tumetoka kuongoza kundi. Tunawaheshimu sana wapinzani wetu lakini malengo yetu ni kuhakikisha tunasonga mbele.
“Tulipoteza mechi mwaka 2021 kwa sababu hatukuwa tayari. Ziko sababu nyingi nyuma zilizosababisha tukapoteza mchezo ule.
“Kwa sasa tuna timu tofauti na Rivers pia wamebadilika, hivyo tunategemea pia utakuwa mchezo Tofauti,” aliongeza Nabi.
Kwa upande wa Morisson alisema, “Malengo yetu ni kuiwakilisha Yanga na Tanzania kwa ujumla. Hatuko hapa kwa sababu ya kujifurahisha, tuko hapa kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.