Kuelekea Mechi ya Leo...Rungu la CAF Laipa Ahueni Simba SC...Mfungaji wa Wydad Azuiwa

 


HII ni habari njema kwa Simba SC kwamba wapinzani wao Wydad Casablanca ambao tayari wapo Dar es Salaam watakosa huduma ya mshambuliaji wao matata , Bouly Junior ambaye ana kadi tatu za njano. Atakuwa jukwaani tu akifuatilia mechi ya  leo Jumamosi jioni.

Kukosekana kwa Junior bila shaka ni habari njema kwao kwa sababu mshambuliaji huyo ndiye kinara wa kuweka wavuni katika kikosi chao akifunga mabao matatu hadi sasa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ingawa kiufundi timu hiyo ina mastaa wengi wazoefu wa michuano hiyo.

Wydad imefunga jumla ya mabao sita huku Junior akifunga mabao matatu peke yake kama mshambuliaji. Junior pengo lake ni kubwa kwenye kikosi cha Wydad kwa sababu mshambuliaji mwingine aliyefunga kwenye Ligi ya Mabingwa ni Zouhair El Moutaraj ambaye ana bao moja huku beki Arsene Zola na kiungo mkabaji Yahya Jabrane wakifunga bao moja moja .

Wydad ambayo inatumia mfumo wa 4-2-3-1 ni wazi kukosekana kwa Junior kutampa fursa Moutaraj nafasi ya kuanza katika mchezo wa Simba kwani alikuwa ni mchezaji wa kutokea benchi huku Junior akianza, ingawa staa wa Tanzania, Simon Msuva amesisitiza kwamba Simba wawe makini timu hiyo itacheza kwa kujilinda na kupoteza muda.

Junior ameonyesha ukali wa kutupia wavuni kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kundi A akimaliza na mabao matatu huku kati yake mawili akifunga kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya JS Kabylie wakati timu yake ikishinda 3-0.

Moutaraj ambaye anapewa nafasi ya kuanza kwenye mchezo na Simba SC, aliingia akichukua nafasi ya Junior na dakika ya 87 alifunga bao huku timu yake ikishinda 3-0 na kwake likiwa ni bao la kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wydad ikitumia mfumo wa mshambuliaji mmoja Junior anasimama mbele peke yake (mfumo wa 4-2-3-1) lakini wanapocheza mfumo wa 4-4-2 basi husimama na Ayman El Hassouni.

Wakati Junior akikosekana kwa Wydad, Simba SC kwao ni furaha kwani kinara wao wa mabao, Clatous Chama aliyefunga manne yupo fiti asilimia zote kwa ajili ya mchezo huo.

Simba inaingia katika mechi hiyo huku ikiwa na wachezaji wengi waliohusika na mabao tofauti na Wydad kwa sababu yupo Jean Baleke ambaye na yeye ana mabao manne.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad