Kuna Wamorocco 1,146,000 wanaishi Ufaransa. Kuna Wamorroco 766,000 wanaishi Hispania. Katika hawa wanaoishi Hispania yumo mtu anayeitwa Achraf Hakim. Pia yumo mama yake anayeitwa Saida. Wote wawili wamevuma wiki iliyopita katika mitandao mbalimbali duniani.
Kwamba Hakimi ameandikisha utajiri wake mkubwa kwa jina la mama yake hali iliyomzuia mke wake mrembo, Hiba Abouk kuchota nusu ya utajiri wake aliouchuma katika soka. Habari hii imeyumbisha dunia na imesababisha zogo kubwa.
Sina uhakika wa asilimia zote kama ni habari ya kweli lakini sishangazwi kama habari yenyewe itakuwa ya kweli. Kuna pande mbili hapa. Kwanza kabisa kuna wanaume ambao ni watoto wa mama. Huwa hawaruhusiwi kukua mbele ya mama.
Wengine ni kwa sababu ya maisha waliyopitia. Unakuta mwanamume analelewa na mama peke yake kwa muda mwingi wa maisha yake. Zaidi ya yote, katika historia ya Hakimi, ameishi maisha ya dhiki na mama yake. Sasa hivi ni muda wa kufurahia utajiri wake na mama yake.
Yeye sio wa kwanza kuwa katika hali hii, wapo wengi. Wasanii, wacheza filamu, wanasoka, wanasiasa na watu wa kada mbalimbali. Wapo ambao walilelewa katika maisha ya mama mmoja ambaye anahaha kumtunza mwanae. Mambo yakibadilika mtoto anahakikisha mama anakula matunda.
Lakini subiri kwanza. Kuna hili la jambo la pili ambalo ni muhimu. Unajua kwa nini wanasoka wengi waliozaliwa Ulaya wenye asili ya Morocco, Algeria na Tunisia wanaamua kucheza nyumbani? Hawa ni kama Hakimi mwenyewe ambaye amezaliwa Madrid, Marouane Chamakh, Riyad Mahrez na mamia wengine.
Hawa wanacheza nyumbani kwa sababu ingawa wamezaliwa Ulaya lakini kule Ulaya wanaishi katika jamii zao. Wanalelewa na jamii zao, wapo Ulaya lakini wanaishi kama vile wapo Tunis, Casablanca, Rabat, Algiers na miji mingine ya kwao.
Hakimi asingeshindwa kucheza katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania. Nani angemweka benchi katika nyakati hizi? Dani Carjaval? Sidhani. Riyad Mahrez angeshindwa kukipiga katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa? Hapana.
Hawa waliamua mapema tu kukipiga katika timu za baba na babu zao. Kwa mfano, Hakimi ameanza kuichezea timu ya Morocco chini ya umri wa miaka 17. Akasogea zaidi na zaidi na mpaka sasa ni tegemeo katika kikosi cha Ufaransa. Ni kama ilivyo kwa Sofiane Amrabat na wachezaji wengi wa kikosi cha Morocco ambao wamezaliwa Ulaya.
Wengine huwa wanahisi kucheza katika timu za taifa za Ulaya ni kama usaliti hivi. Unaamka katika nyumba ambayo imejaa Wamorocco, majirani zao wote Wamorocco, halafu unaichezea timu ya taifa ya Ufaransa. Ni kitu ambacho kwao wanaona hakijakaa sawa.
Ni basi tu wanajikuta wapo Ulaya lakini wanakulia katika misingi ile ile ambayo wangeweza kukulia kama wangezaliwa katika miji yao ya nyumbani Afrika. Haishangazi kuona hawaingii katika uzungu sana na badala yake wanajikita katika misingi yao ya Kiarabu.
Wanaongea Kiarabu na Kifaransa ingawa lugha yao ya kwanza ilipaswa kuwa Kifaransa kwa sababu shuleni wanasoma na watoto wa Kizungu. Wanafundishwa kuswali swala tano kama kawaida. Ifikapo wakati wa mfungo huwa wanafunga kama kawaida.
Nimeshuhudia hili nikiwa katika miji kama Madrid, Barcelona, Paris, Antwerp na kwingineko. Nimeshuhudia pia kwa rafiki zangu wa pale Genk pindi nikimtembelea staa wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anayecheza pale.
Rafiki yangu pale anaitwa Noureddine. Ni Mbelgiji ambaye ana asili ya Morocco. Anaishi kama vile yupo Casablanca. Haishi kama mtoto wa kizungu. Matokeo yake, heshima yake kwa wazazi wake inabakia pale pale na ameendelea kuwa mtoto wa mama.
Ni kitu tofauti na watoto wa kizungu ambao mara nyingi wakishafikisha umri wa miaka 18 uhusiano wa karibu na wazazi unapungua kwa sababu jamii yao inampa mamlaka makubwa ya kuchukua maamuzi yake binafsi.
Ukichunguza zaidi kwa wachezaji wa kizungu utasikia stori nyingi za yeye na mpenzi wake na sio stori nyingi kuhusu yeye na mama yake au yeye na baba yake. Hawana Hakimi wanaishi Kiafrika hasa pale Ulaya na huwa hawakui kama ilivyo kwa wanasoka wazungu au wanasoka weusi ambao wamezaliwa Afrika au Ulaya.
Ndio maana haishangazi kuona stori za wachezaji weusi au wazungu kufilisiwa na wanawake zipo nyingi kuliko stori za wachezaji wa Kiarabu. Ni kwa sababu kama hii ya Hakimi. Wanakulia katika matunzo yenye maadili kutoka katika familia hadi katika jumuiya.
Tatizo kubwa la watoto hawa wa Kiarabu ni watundu sana. Ni kama ilivyo kwa watoto wa Kiarabu wa Kariakoo na kwingineko. Utundu mwingi na wakati mwingine wanapitiliza. Vurugu nyingi za usiku ambazo wakati mwingine zinasababisha kuharibu maisha yao ya soka.
Wengi ni masela tu ingawa wana maadili. Yuko wapi Samir Nasri? Vipi kuhusu Hatem Ben Arfa? Vipi kuhusu kile kichwa ambacho Zinedine Zidane alimpiga Marco Materrazzi katika kombe la dunia mwaka 2006? Ilikuwa mechi yake ya mwisho katika soka.
Ukorofi huu wa hawa ndugu zetu ndio ambao ulisababisha Wamorocco wanaoishi Ubelgiji kufanya vurugu baada ya Morocco kuifunga Ubelgiji katika kombe la dunia. Ilinishangaza sana. Wao ndio wameshinda halafu wao ndio wanafanya vurugu.
Ingekuwa wao ndio ambao wamedhulumiwa tungeweza kudai kulikuwa na hila dhidi ya Waarabu katika michuano yenyewe. Lakini hawakupoteza mechi na bado wakafanya vurugu dhidi ya wazawa. Inashangaza kidogo.