GUMZO kwa mashabiki wa Yanga kwa sasa ni kuona wanaiondoa timu ya Rivers United kutoka Nigeria ambayo wamepangwa kukutana nayo katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuona wakitinga hatua ya nusu fainali.
Jambo ambalo mashabiki wa Yanga ambalo linawafanya kutaka kuwatoa Rivers United ni kutaka kulipiza kisasi kutokana na kumbukumbu za kutolewa katika Ligi ya Mabingwa misimu miwili iliyopita na timu hiyo.
Safari hii miamba hiyo inakutana tena ambapo Championi Jumamosi linakupa sababu 5 za Yanga kuweza kupata matokeo mazuri na kuwaondoa Rivers katika robo fainali hiyo kama ifuatavyo.
KULIPA KISASI
Kama ambavyo inafahamika hili ndio jambo kubwa ambalo mashabiki wa Yanga, viongozi na hata wachezaji wameweza kulizungumzia baada ya kupangiwa Rivers United kutaka kulipa kisasi
Hii inatokana na msimu uliopita Yanga kuondolewa na timu hii katika hatua ya awali ya ligi ya mabingwa Afrika, hivyo watautumia mchezo huu kutaka kulipa kisasi.
UBORA WA KIKOSI CHA YANGA
Kikosi cha Yanga kwa sasa kimeongezeka ubora katika kila idara jambo ambalo linaifanya Yanga kuwa moja kati ya timu tishio kwa sasa kwenye michuano hii.
Ukikitazama kikosi kile kilichocheza na Rivers United kwa msimu uliopita ni tofauti kabisa na kikiwa na maongezeko ya wachezaji wengi kama Stephane Aziz Ki, Benard Morrison, Kennedy Musonda, Mudathir Yahya, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ na wengineo.
UZOEFU KIMATAIFA
Yanga kwa sasa wamepata uzoefu wa michuano hii ya kimataifa na tofauti na misimu miwili nyuma au hata walivyoanza msimu huu, ukiangalia kwa jinsi ambavyo wameanza kupata matokeo ugenini na nyumbani hiyo ni ishara tosha.
Yanga hapo mwanzo walionekana kupata shida katika kuutumia hata uwanja wa nyumbani haswa kwatika michezo miwili dhidi ya Al Hilal na Club Africain ambayo yote walishindwa kupata matokeo.
Tofauti na sasa ambapo kwenye makundi wameshinda michezo yote mitatu ya nyumbani.
KUMALIZIA MECHI NYUMBANI
Kitendo cha Yanga kumalizia mechi nyumbani ni faida kubwa sana kwao kwa kuwa watakuwa na nafasi kubwa ya kusawazisha makosa kama watakuwa wameyafanya katika mchezo wa awali Nigeria.
Yanga wanapata faida hiyo kutokana na kumaliza wa kwanza katika kundi lake tofauti na Rivers United.
BENCHI LA UFUNDI
Mara ya kwanza ilionekana benchi la ufundi la Yanga wanashindwa kuzicheza mechi za kimataifa lakini kupitia kocha Nasreddine Nabi mambo kwa sasa yapo vizuri.
Pia msaidizi wake, Cedric Kaze ameonekana kufanya vyema ambapo kupitia mchezo dhidi ya TP Mazembe, Nabi alikosekana lakini kila kitu kilikuwa sawa.
Stori na Marco Mzumbe