Babati. Mtoto Justin Kiluso (5) amenusurika kuliwa na wanyama wakali baada ya kupotea katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa siku mbili, alipokuwa akichunga ng'ombe na wenzake katika kijiji cha Kakoyi kilicho jirani na hifadhi hiyo.
Mtoto huyo alipotea Jumapili Aprili 9, saa 7 mchana hifadhini humo, hata hivyo alipatikana Jumanne iliyopita akiwa na hali mbaya kutokana na kukosa chakula kwa siku mbili.
Hayo yalibainika jana baada ya Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), kutembelea Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na USAID, unaolenga kuimarisha uhusiano mwema kati ya binadamu na wanyamapori katika ushoroba wa Kwakuchinja.
Akisimulia mkasa huo, Mwenyekiti wa kijiji cha Kakoyi, Loishiye Elias alisema alipokea taarifa za kupotea kwa mtoto huyo jioni, baada ya wazazi wake kurudi kutoka mnadani na kuambiwa mtoto wao haonekani tangu mchana.
Loishiye alisema siku iliyofuata (Jumatatu), walipiga mbiu na wanakijiji kutoka vijiji vinne vya Mswakini, Olasiti, Minjingu na Kakoyi waliingia porini kuanza kumsaka mtoto huyo bila mafanikio.
"Watu kama 600 waliingia porini kumtafuta mtoto huyo. Tulipata msaada wa magari kutoka kwa mwekezaji, kampuni ya ChemChem lakini hatukumuona. Tulifika hadi kwenye mpaka na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire," alisimulia kiongozi huyo.
Alisema walianza kumsaka tangu Saa 12 alfajiri hadi saa 2 usiku, baadaye waligundua upande walioelekea ulikuwa tofauti na kule alikokuwa mtoto.
Mwenyekiti huyo alisema siku iliyofuata (Jumanne), walipigiwa simu kujulishwa kwamba mtoto kaokotwa na askari wa wanyamapori akiwa ameishiwa nguvu kwa kukosa chakula.
"Tunamshukuru Mungu kwa kuwa maeneo aliyopita ni hatari, yana wanyama wakali na askari walituambia kwamba mita 200 kutoka pale alipookotwa kulikuwa na kundi la simba," alisema.
Loishiye alisema baada ya kupatikana, alipatiwa uji kama huduma ya kwanza na kupelekwa kituo cha afya cha Ngaiti na ilibainika kuwa sukari yake imeshuka.
Hata hivyo, Loishiye alisema matukio kama hayo yaliwahi kutokea miaka ya nyuma na la hivi karibuni ni la mwaka 2020, mtoto wa miaka saba naye alipotea porini, lakini alipatikana siku hiyohiyo. "Huenda huyu mtoto hakudhuriwa na wanyamapori kwa sababu tumezoeana, hata huko machungani tumekuwa tukipishana nao, kwa hiyo huenda wanyama walimwona lakini wakaendelea na mambo yao.
Baba mzazi azungumza
Akizungumzia hali ya mwanaye, baba mzazi wa mtoto huyo, Semari Kiluso alisema waliruhusiwa kutoka hospitali Alhamisi iliyopita na anaendelea kunywa dawa alizopatiwa.
Alisema Justine alimweleza kwamba alikutana na fisi lakini alimtisha kwa fimbo akakimbia. Pia, alisema aliwaona simba ambao walimpita bila kufanya kitu.
Mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori katika eneo hilo unaelezwa kwamba umekuwa mzuri kwa kipindi kirefu kwa sababu wanaishi na wanyama hao na hata wanapovamia makazi yao, wamekuwa hawasababishi madhara makubwa.
Kwa upande wa Chifu wa kabila la Wamasai katika kitongoji cha Eluwayi kilichopo katika kijiji cha Olasiti, Leteiva Loburu alisema simba wa Tarangire siyo wachokozi ukilinganisha na wa Manyara.
Alifafanua kuwa mnyama mkorofi zaidi ni fisi ambaye amekuwa akifanya uharibifu. “Fisi mmoja alivamia zizi na kuua mbuzi 24 lakini hakula hata mmoja, akaondoka zake.”
Chifu huyo alibainisha kuwa siku hizi ushujaa wa kijana wa Kimaasai siyo kuua simba kama zamani, wengi wamepata elimu na kubadilisha tabia zao na kuwaona wanyama hao kama rafiki zao wanaohitaji kutunzwa na siyo kuwindwa.