Dar es Salaam. Wakati kukiwa na kauli tofauti kuhusu suala la mabasi kusafiri usiku, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), imesema hata ukifanyika uamuzi huo, bado kuna madhara kutokana na barabara nyingi kutokuwa na taa.
Desemba 2022 mamlaka hiyo ilisema inatarajia kuruhusu mabasi ya mikoani kufanya safari zake kwa saa 24 ili kukabiliana na ongezeko la abiria mwishoni mwa mwaka.
Kauli hiyo ya Latra ilitolewa ikiwa umepita mwezi mmoja tangu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliposema haoni tatizo magari ya abiria kufanya safari usiku kama magari mengine yanafanya hivyo.
Dk Tulia alisema hatua ya kuyazuia magari usiku inarudisha nyuma maendeleo kiuchumi na kutaka wanaohusika kuangalia upya utaratibu huo kama kuna kikwazo kitafutiwe ufumbuzi.
Tofauti na Dk Tulia, kauli za kuruhusu mabasi kutembea usiku zimeendelea kutolewa mara kwa mara na baadhi ya viongozi.
Mfano Julai, 2019 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nchini, Kangi Lugola alipiga marufuku makamanda wa polisi wa mikoa kuyazuia mabasi kusafiri usiku kwa kisingizio cha kuhofia kuvamiwa na majambazi.
Lakini Aprili 4, mwaka huu, mjadala huo uliibuka tena bungeni baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Janeth Masaburi (CCM), kutaka kujua ni lini Serikali itatunga sheria kali za kuwadhibiti madereva wazembe.
Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alihoji ni kwa nini Serikali iendelee kuzuia mabasi ya abiria kusafiri usiku.
Kutokana na hoja hiyo, Spika wa Bunge alihoji tena sababu zinazozuia mabasi kusafiri usiku, kwa kipindi hicho ambacho Serikali imejenga na inaendelea kufanya maboresho makubwa ya miundombinu nchini.
“Pamoja na majibu ya Serikali hakuna maana ikiwa Serikali inajenga miundombinu, halafu suala la kusafiri usiku linakuwa tatizo, badala ya kuweka mazingira rafiki kwenye usafirishaji huo,” alisema Dk Tulia.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo alisema kwa upande wa mamlaka hawana tatizo kwa kuwa wameshatoa vibali kwa magari maalumu kufanya safari za usiku kama majaribio.
“Tukifanikiwa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani litaangalia uwezekano wa kuruhusu magari hayo kusafiri kwa saa 24,” alisema
Kauli iliyowahi kutolewa na Jeshi la Polisi
Septemba 2022 aliyekuwa Kamanda wa Kikosi Cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa alisema kuhusu mabasi kusafiri usiku, mamlaka za juu zinaendelea kulijadili suala hilo.
Alisema katika kipindi hicho, madereva wanapaswa kufuata utaratibu uliotolewa na Latra.
“Hilo jambo linajadiliwa katika mamlaka mbalimbali, kuangalia sababu za kiusalama za watu na mali zao,” alisema Mutafungwa.
Uamuzi wa kuyazuia mabasi kusafiriki usiku ulitangazwa mwaka 1992 na aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela baada ya ajali za usiku kukithiri nchini.
Kauli ya Serikali
Akizungumzia hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini alisema magari ya abiria hayaruhusiwi kusafiri usiku zaidi ya saa sita na wenye magari ya abiria walishaelekezwa kuweka ratiba zao ili kuendana na muda.
Aliitaja baadhi ya mikoa ikiwemo Tabora na Katavi kuwa magari hayaruhusiwi kutembea usiku kutokana na mazingira yake ya kiusalama.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Joseph Priscus alisema kuwa ushauri uliotolewa na Spika wa Bunge ni wa muhimu kuzingatiwa ili kukuza uchumi.
Alisema hakuna haja kuruhusu gari kumaliza safari usiku na kukataza kuanza safari muda huo.
Alisema suala hilo lina athari kwa uchumi, hasa ukizingatia wafanyabiashara hawana muda maalumu wa kusafiri.
“Ni wakati wa Serikali kuangalia utaratibu wa kuruhusu magari kuanza safari usiku, tatizo sio kutembea usiku, hapa tunachoangalia ni muda wa kuanza safari,” alisema Priscus.