Majeruhi watano ajali ya bajaji, IST wafariki dunia



Iringa. Majeruhi watano kati ya sita wa ajali iliyohusisha bodaboda, bajaji na gari dogo aina ya IST wamefariki dunia leo wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Majeruhi hao walipata ajali jana Aprili 25, 2023 katika eneo la TRM, Kihesa Kilolo, Manispaa ya Iringa.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Alfred Mwakalebela amesema majeruhi mmoja bado anaendelea kupatiwa matibabu ili kuokoa uhai wake.

"Watu watatu walifariki tangu jana, vifo viwili vimetokea leo wakati matibabu yakiendelea kufanyika," amesema Mwakalebela.


Aidha Mwakalebela amesema mpaka sasa majeruhi mmoja anayeendelea kupatiwa matibabu bado hajajulikana anapotokea na ndugu hawajajitokeza.

"Inasemekana kuna kijana haonekani anafanya kazi ya kukatisha tiketi Kihesa, sasa nashauri watu jirani wangekuja wamuone kijana huyu huenda akawa ni yeye," amesema Mwakalebela.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi juu ya chanzo cha ajali hiyo.


Hata hivyo baadhi ya mashuhuda wamesema bodaboda iliyoingia barabarani ghafla akitokea njia ndogo ndiyo sababu ya ajali hiyo.

Aidha wakazi jirani wa eneo la tukio wamesema mara nyingi ajali zinazotokea chanzo huwa ni mwendokasi wa madereva hivyo wanaomba Jeshi la Polisi na madereva kuwa makini wawapo barabarani.

"Hawa bodaboda muda mwingine wanaendesha bila hata ya kuwa na uoga na kujionea huruma ona sasa kilichotokea kwa dakika chache tu,”amesema  Rashid Msuva.

Baadhi ya ndugu wa marehemu Lilian Malila, Mkazi wa Nduli wamesema  kesho Aprili 27, 2023  wanatarajia kumzika.


"Labda ni mipango ya Mungu tu japokuwa kaacha watoto wadogo, makazi yake yalikuwa ni Mbeya, huku alikuja tu kumuuguza mama yake kumbe yeye ndo anatangulia," amesema Lucia Jafary, mmoja Kati ya ndugu zake.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad