BARAZA la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO), limeanza kuyahoji mashirika 29 yasiyo ya kiserikali (NGO), dhidi ya tuhuma iliyoibuliwa na waziri wa zamani, Dk. Harrison Mwakyembe na baadaye kusambaa kwenye mitandao ya kijamii alizodai zinajihusisha na kampeni ya kueneza ushoga nchini.
Mwakyembe ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali kwenye serikali ikiwamo Waziri wa Katiba na Sheria, alitoa taarifa hiyo kwenye mkutano ulioandaliwa na viongozi wa dini kupinga mapenzi ya jinsia moja uliokuwa na kaulimbiu ‘Tanzania bila ushoga inawezekana’.
Kwenye taarifa yake, alisema utafiti walioufanya kupitia tume aliyoiunda umebaini kuna mashirika 29 yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na vitendo vya kueneza mapenzi ya jinsia moja (ushoga), jambo ambalo ni kinyume na maadili ya kitanzania.
Kupitia tamko hilo lililogusa hisia za watu wengi na kuzua gumzo kwenye mitandao ya kijamii, Mwenyekiti wa NaCoNGO, Lilian Badi alisema baada ya kuona taarifa hiyo kuna hatua kadhaa walizichukua kukabiliana na kilichoibuliwa.
“Tumeyaita na kuanza kuyahoji hayo mashirika yaliyotuhumiwa na kufanya uchunguzi wa kina na tunamuhoji Dk. Mwakyembe ili tujue alifanyaje utafiti wake mpaka akabaini uwapo wa NGOs 29 zinazoshinikiza ushoga.”
“Tulifanya kikao cha dharura cha kamati tendaji kujadili namna ya kuchunguza hali hiyo na kuweka maazimio ya utekelezaji, kufanya mawasiliano ya awali na mashirika yote yaliyotuhumiwa kupitia utafiti huo ikiwa ni maandalizi ya kuwafanyia uchunguzi pamoja na mahojiano ya kina,” alisema Dk. Lilian na kuongeza:
“Hatua nyingine, tumeomba kukutana na kamati ya Dk. Mwakyembe ili tupatiwe taarifa yao itusaidie kuendeleza maoni yetu na juhudi tutakazozichukua kama viongozi wa sekta na NGO.”
Alisema baada ya kukamilisha hatua hizo, wataandaa taarifa ya pamoja itakayoambatana na tamko kwa umma kuweka hadharani hatua watakazo zichukua.
Alitahadharisha kuwa ni vyema kutambua suala hilo ni mtambuka sio NGO pekee wanaohusika, hata serikali pia kupitia vyombo vyake, wabia wa maendeleo na makundi mengine ambayo hayajatajwa moja kwa moja na kwamba busara inahitajika katika kushughulikia sakata hilo.
“Tunataka kulinda jamii yetu, tuna kiu ya kubaki salama suala hili lipo kinyume cha maadili ya kitanzania, ni vyema tuungane pamoja kuliko kujigawa kama baadhi ya taarifa zilizosambaa zinamweleko wa kunyooshea vidole baadhi ya makundi.”
Pia aliwataka wamiliki wa mashirika hayo kuepuka kuhukumu baadhi ya makundi au taasisi mpaka pale watakapokuwa na taarifa kamili au kuthibitika bila mashaka kama kundi fulani limehusika na kashfa hiyo.
Alisema ni vyema mjadala kuhusu suala hilo ungoje taarifa rasmi ya NaCoNGO, kuhusu hali halisi itakayotoa undani wa uchunguzi kwa mashirika yote yaliyohusika na tuhuma hizo, kisha taarifa yao itapelekwa katika bodi ya uratibu kupitia ofisi ya msajili wake iliyopo nchini.