KUFUATIA Bosi wa Yanga, Ghalib Said Mohammed (GSM) kusafiri na Yanga kwenda DR Congo kuishuhudia timu yake ikicheza dhidi ya TP Mazembe, mastaa wa timu hiyo wamefunguka kuwa kitendo kimewaongezea morali ya kupambana katika mchezo huo.
Aidha ukiachana na GSM kusafiri na Yanga pia Rais wa timu hiyo, Hersi Said ni miongoni mwa watu waliopo nchini huko sambamba na Abbas Tarimba ambaye ni kiongozi kutoka kwa wadhamini wao Sportpesa.
Yanga leo Jumapili wanatarajiwa kukipiga dhidi ya TP Mazembe katika mchezo ambao unatarajiwa kufanyika ugenini, mchezo ambao kama Yanga watapata ushindi mzuri basi watajihakikishia nafasi ya kubaki kileleni.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele alisema: “Kitendo cha bosi wetu kuja huku kinatupa hamasa kubwa sana sisi kama wachezaji ya kupambana kuhakikisha kuwa tunapata matokeo na tusimuangushe kiongozi wetu.
Rais wa Yanga, Hersi Said (kushoto) na Makamu wa Rais wake Arafat Haji (kulia) wakiwa na Ghalib Said Mohammed (GSM).
“Hivyo tutapambana kuhakikisha kuwa tunashinda, tunafahamu kuwa ni mchezo mgumu lakini tupo tayari kuupigania mchezo huu ili tuweze kutimiza malengo yetu,” alisema mchezaji huyo.
Naye beki wa kati wa Yanga, Dickson Job alisema: “Sisi kama wachezaji hakika tumepata moyo wa kupambana kuona bosi wetu amekuja kutuangalia tukicheza na sisi kama wachezaji tunamuahidi ushindi mkubwa.”
WASAKA REKODI 3
Katika mchezo huo, Yanga wenyewe watakuwa wanasaka rekodi tatu tofauti ambazo zitawafanya kuongeza ukubwa wao ndani ya Afrika.
Rekodi ya kwanza ni ya kumaliza kileleni mwa msimamo wa kundi lao ambapo kwa sasa wapo pointi sawa na Monastir, ya pili kushinda ugenini mbele ya Mazembe na ya tatu kuingia robo fainali kwa kishindo kama watafanikiwa kushinda mechi hiyo.
Stori na Marco Mzumbe