MABOSI wa Simba, juzi walimpa kipa wao namba tatu, Ally Salim shilingi milioni 10 kama sehemu ya ahadi endapo asiporuhusu bao katika mchezo wa Kariakoo Dabi.
Dabi hiyo ilizikutanisha timu kongwe za Simba dhidi ya Yanga, ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, kipa huyo alionesha ubora wa kupangua na kuzuia mashuti mawili ya mshambuliaji tegemeo wa Yanga, Mkongomani Fiston Mayele.
Mmoja wa Mabosi wa timu hiyo, kutoka Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, ameliambia Spoti Xtra kuwa, kipa huyo kabla ya mchezo alipewa ahadi hiyo ya fedha.
Bosi huyo alisema kipa huyo alipewa ahadi ya kufikisha ‘clean sheet’ ya pili watakapocheza dhidi ya Yanga ambayo aliitimiza kwa kuokoa michomo golini kwake.
Aliongeza kuwa, kipa huyo alikabidhiwa fedha hizo mara baada ya mchezo huo ambao ulimalizika kwa Yanga kufungwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Hennock Inonga na Kibu Denis.
“Kabla ya mchezo wa Kariakoo Dabi, Salim alikaa kikao na viongozi mara baada ya yeye kuchaguliwa kuanza katika kikosi cha kwanza.
“Katika kikao hicho, aliwekewa mtego wa kutoruhusu bao katika mchezo wa dabi dhidi ya Yanga ili afikishe clean sheet ya pili baada ya ile dhidi ya Ihefu.
“Hivyo baada ya kuifikisha clean sheet hiyo ya pili, uongozi umempatia bonasi hiyo Salim kwa ajili ya kumuongezea morali ya kupambana katika michezo ijayo ya ligi na Kombe la FA,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kuwa: “Salim anastaili pongezi kubwa kutokana na kiwango bora ambacho amekionesha katika mechi kubwa.
“Haikuwa mechi nyepesi kwetu, akicheza mechi ngumu ya dabi, alionesha kiwango bora akiwazuia washambuliaji kama kina Mayele kushindwa kufunga mabao.”
STORI NA WILBERT MOLANDI