Mbunge Chadema watolea uvivu wabunge wa CCM bungeni




Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kwa tiketi ya Chadema
MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, (Chadema), Aida Khenani, amewataka baadhi ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), “waache unafiki” ili wamsaidie Rais Samia Suluhu Hassan, katika kufikia malengo yake ya kuliletea taifa maendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Khenani ametoa wito huo leo tarehe 4 Aprili 2023, akichangia hoja ya ya azimio la Bunge kumpongeza Rais Samia kwa kuimarisha demokrasia na kukuza demokrasia ya uchumi, bungeni jijini Dodoma.

“Maridhiano yanayoendelea ni afya kwa taifa ili lifike uchumi tunaofikiri, ni lazima turuhusu mawazo mbadala maana utayapima kama yana maslahi kwa taifa utayatumia. Naunga mkono azimio hili endapo sisi Bunge tutamsaidia Rais, lakini tukikaa kwenye unafiki hatuamsaidia Rais,” amesema Khenani.

Akichangia azimio hilo la kumpongeza Rais Samia kwa kuimarisha demokrasia, Khenani amehoji wabunge wa CCM msimamo wao ni upi kwa kuwa kipindi mikutano ya hadhara inafungiwa walipiga makofi bungeni kupongeza hatua hiyo na sasa wanapiga makofi kumpongeza Rais Samia kwa kuifungua.


“Kuhusu kukuza demokrasia Napata mazingira magumu sana kwamba ni kweli amekuza demokrasia lakini amekuza demokrasia iliyodhohofishwa na nani na wa chama gani? Tunapozungumza mikutano ya hadhara yalizungumzwa hapa na Mwigulu kwamba lazima tutenge muda wa kufanya kazi na muda wa mikutano tulipiga makofi,” amesema Khenani.


Khenani amehoji “wabunge wa ndani ya Bunge hili leo tunapongeza kurudisha mikutano ni kweli tunapongeza kurudisha lakini nani aliondoa na wa chama gani? Sisi wabunge tunasimama wapi?”

Katika hatua nyingine, ameishauri mchakato wa marekebisho ya katiba uanze mara moja, ili kuenzi mambo mazuri yanayofanywa na Rais Samia hata kipindi ambacho ataondoka madarakani.

“Ili tufikie malengo ya maridhiano ambayo Rais ameongoza lazima kuwepo katiba mpya, Rais ameonyesha CCM mko tayari lazima mchakato huu uanze mara moja kusimamia yale anayozungumza ili atakapokuja Rais mwingine afuate misingi ambayo katiba mpya itakuwa imeweka,” amesema Khenani na kuongeza:

“Leo anapongezwa hapa, akija mwingine atakubali hiyo mikutano au ataondoa tena wakati iko kwa mujibu wa sheria? Lazima msingi inayowekwa leo kwenye utawala bora ije isimamiwe na yeyote atakaepata nafasi hiyo.,”

Mbunge wa Mafinga Mjini kupitia CCM, Cosato Chumi, amejibu hoja wa Khenani iliyohoji kubadilika kwa msimamo wao akisema hatua hiyo inatokana na mazingira kubadilika.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad