Dar es Salaam. Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama, Dar es Salaam wamehimizwa kumtegemea Mungu na kuacha kulinda makaburi ya wengine, huku wakihimizwa kutambua umuhimu wa watu wenye pesa (matajiri) kwenye Injili.
Akihubiri katika ibada ya Pasaka kanisani hapo, leo Jumapili, Aprili 9, 2023 Mchungaji Eliona Kimaro, amesema baadhi ya nchi nyingi za Kiafrika zinawapa majina ya ajabu matajiri, lakini ni watu wenye nguvu ambao Injili inawatambua.
"Wengine wanawaita mafisadi, mara wakwepa kodi na majina ya hovyo, lakini ukifika kwa Yesu anawaheshimu sababu ndiyo waliomzika," amesema mchungaji huyo na kuongeza.
"Ninachokiona ni kiroho papo, mnawaita freemasons na majina mabaya, lakini wana nafasi yao kwenye Injili," amesema mchungaji huyo akimtolea mfano Yosefu wa Arimathaya, aliyekuwa tajiri na kwenda kwa Pilato kuomba mwili wa Yesu auzike.
"Matajiri ndio wanaficha aibu ya kanisa, lakini nao wajifunze kwa Yosefu aliyekuwa amejitengenezea kaburi lake, akaenda kumzika yesu.
"Katika familia zetu, mmoja Mungu akimbariki ndiye anaficha aibu ya familia, lakini tatizo lililopo ni chuki na wivu, utakuta mtu aongei na ndugu yake kisa ni tajiri, ndiyo Mungu amembariki," amesema mchungaji huyo akishangiliwa kwa nguvu na waumini waliokuwa wamefurika kanisani hapo.
Amesema Pasaka hii inapaswa kubadilisha matendo ya watu, akitolea mfano kwamba roho mbaya zilikuwepo tangu wakati wa Yesu.
Mchungaji Kimaro aliyeanza kwa kusoma maandiko katika kitabu cha Wakorintho wa kwanza, 15:12 amesema dunia ina watu wana roho mbaya, lakini mbingu zinawalinda watu wake siku zote.
"Maandiko yanasema, askari baada ya kumuua Yesu waliomba kaburi lake lilindwe can you imagine (embu fikiria).
"Waliona haitoshi, tayari wameshamuua na kwenda kumlinda, ndivyo ilivyo katika jamii yetu, kuna watu wanasema nitahakikisha yule anafukuzwa kazi na aajiriwi popote au nitahakikisha nakitia kitumbua mchanga hakitafuniki, katika Pasaka ya mwaka huu, hakikisha hulindi makabuli ya watu," amesema.
Mchungaji huyo alitania kwamba siku hizi, ukimwaga mboga, basi mwingine anaondoa jiko kabisa sio kumwaga ugali.
"Utakuta mtu yuko Mwanza, wewe huko Dar es Salaam, hamkutani, lakini analinda kaburi lako, nguvu ya ufufuo ipo," amesema mchungaji huyo.