Jeshi la Polisi nchini Kenya limemkamata Mchungaji Hellen Wanjiru Weri (62) wa kanisa la Army Rurwama Fellowship la mjini Nakuru, kwa tuhuma za kuwafungisha baadhi ya waumini kwa wiki moja bila kula wala kunywa chochote, ili sala zao ziweze kupokelewa mbinguni.
Mchungaji Wanjiru ambaye hujitambulisha kama mama wa kiroho wa mataifa yote (Spiritual mother of all Nations) aliwakusanya waumini 32 nyumbani kwake katika kijiji cha Kihingo, kaunti ya Nakuru kwa huduma ya maombezi, ambapo kwa wiki moja waliyokaa hapo hawajala wala kunywa chochote.
Kutokana na kuzidiwa njaa kwa muda mrefu baadhi ya waumini hao walizirai, na wengine kupoteza nguvu za kuendelea na maombi lakini Mchungaji Wanjiru aliwasisitiza waendelee kuomba. Waumini wote walinyang'anywa simu na kuzuiwa kuwasiliana na ndugu zao wakati wote wa maombi hayo yaliyopangwa kufanyika kwa siku 14.
Mama Wanjiru aliwaambia waumini wake ikiwa Yesu alifunga kwa siku 40 bila kula wala kunywa ili aushinde ulimwengu, nao watafunga kwa siku 14 na watashinda matatizo yao yote yanayowakabili.
Wanjiru amekamatwa baada ya mwanamke mmoja huko Nakuru kudai kuwa binti yake aliacha kazi katika kampuni moja ya mawasiliano na kwenda kwa Mama huyo kwa ajili ya maombi na kufunga na hakurudi tena nyumbani. Polisi walipofuatilia walimkuta binti huyo na wenzake 31 nyumbani kwa Wanjiru wakiwa kwenye hali mbaya kiafya na wamedhoofu.
Waumini hao wamelzwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti hiyo (Nakuru Level 6 Hospital) kwa msaada wa dharura wa kiafya. Ofisi ya DCI imesema inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, ikiwa ni siku chache zimepita tangu tukio jingine la kufanana na hilo kutokea huko kaunti ya Kilifi likimhusisha Mchungaji Paul Mackenzie na kusabanisha vifo vya zaidi ya watu 100.