Miss Rwanda afichua jinsi Thabo Bester, mpenzi wake walivyojaribu kumtapeli



Johannesburg. Maovu mengine ya Thabo Bester yanazidi kufichuliwa baada ya aliyekuwa Miss Rwanda mwaka 2016, Jolly Mutesi kueleza jinsi Thabo na mp-enzi wake, Dk Nandipha Magudumana walivyojaribu kumshawishi kwenda Cape Town kwenye kipindi bandia cha Netflix wakiwa na lengo la kumtapeli.

Inadaiwa kipindi hicho kilikuwa kinatarajiwa kuwa na mastaa maarufu kama vile Kylie Jenner na mwanamuziki Drake kutoka nchini Marekani.

Tovuti ya IOL ya nchini Afrika kusini inasema Mutesi alifuatwa na kampuni ya Arum Holdings ambayo ilimtaja Dk Nandipha (ambaye ni mpenzi wa Thabo) kuwa Mkurugenzi Mtendaji wake na Thabo, kwa jina la TK Nkwana, kuwa mwenyekiti.

“Kwa wachache wanaonifahamu vizuri wanajua kuwa mimi ni mtu wa kujivinjari. Hivyo, Septemba mwaka jana, nilipata mwaliko wa kwenda Afrika Kusini kama mgombea anayeweza kuandaa kipindi cha Netflix pamoja na Kylie J, Drake,” anasema Mutesi.


Mutesi ambaye pia ni mjasiriamali amesema alihoji kwanini walimchagua yeye, kampuni hiyo ilijibu kwamba walihitaji mtu wa Afrika Mashariki kwa ajili ya onyesho hilo na inaonekana yeye ndiye alikuwa mwenye sifa.

Mrembo huyo amesema alikuwa na mashaka licha ya kufurahishwa na fursa hiyo ambayo ingeweza kumpa jukwaa kubwa la kujitangaza ulimwenguni, pamoja na kandarasi ya miaka mitatu ambayo angelipwa Dola za Marekani 3 hadi 4 milioni ikiwa ni zaidi ya Sh9 bilioni kwa mwaka.

“Nafsi yangu iliniambia niichunguze kampuni hiyo. Niliomba wasifu wa kampuni, mwaliko rasmi na uhifadhi wa hoteli, nikawasilisha kwa mamlaka ili kutafuta ushauri na kunisaidia kujua jinsi ilivyokuwa halali,” ameeleza.


Amesema uchunguzi ulifanyika na alishauriwa asiende kwa sababu kila kitu kilichopatikana kuhusu kampuni hiyo kilikuwa cha ulaghai.

Mutesi alitoa shukrani zake kwa Ubalozi wa Rwanda nchini Afrika Kusini kwa kuokoa maisha yake kutoka kwa Thabo na Dk Nandipha. Amewatahadharisha vijana kufanya utafiti kwanza kuhusu fursa zozote zinazotolewa kwao.

“Wapendwa vijana, hasa wale wanaopenda kung’ara, tafadhali kuweni makini kwenye fursa yoyote. Sio vyote vinavyong’ara ni dhahabu, kuna mafisadi wasio na huruma, tafuta ushauri kila wakati,”ameshauri Mutesi.

Thabo na mpenzi wake Dk Nandipha bado wanashikiliwa na Polisi nchini Afrika Kusini kufuatia kukamatwa kwao jijini Arusha nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad