Shinyanga. Mkuu wa Shule ya Sekondari Imenya Kata ya Itwangi Halmashauri ya Shinyanga, Seleman Karavina amesimamishwa kazi kwa madai ya kumpeleka mganga wa kienyeji shuleni hapo kupiga ramli chonganishi.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu ya mwaka Aprili 28, 2023, Diwani wa Kata ya Itwangi, Sonya Jilala amesema uamuzi wa mwalimu huyo ni baada ya baadhi ya wanafunzi kudaiwa wana mapepo kutokana na kuanguka hovyo na kupiga kelele.
Amesema hali hiyo ilizua taharuki shuleni hapo ndipo mwalimu huyo akampeleka mganga wa kienyeji kupiga ramli chonganishi ambayo iliwatuhumu baadhi ya wazazi kuhusika kufanya vitendo vya kishirikina.
“Haya mambo yametokea hivi karibuni ambapo mwanafunzi mmoja wa kidato cha pili aliandikiwa barua na watu wasiojulikana akituhumiwa yeye na wazazi wake ni washirikina watauawa” amesema Mhela
Kufuatia vitendo hivyo vya kishirikina, Diwani huyo alimuomba Mkuu wa Wilaya kuitembelea shule hiyo na kuwatoa wasiwasi wazazi na wanafunzi kutokana na mambo yaliyokuwa yakifanywa na mwalimu huyo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Nice Munissy amesema amemsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili huku akiwaonya watumishi wa umma kutojihusisha na vitendo hivyo.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari, Clensensia Jogopa ameahidi kufuatilia suala hilo na kuchunguza ili kujua kilichokuwa kinaendelea.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi amewataka madiwani kutosubiri baraza la madiwani ndipo waseme matatizo yanayotokea katika maeneo yao kwakuwa mengine yanahitaji kushughulikiwa haraka.
“Nikitoka kwenye kikao hiki nikiwa naelekea ofisini nipate taarifa rasmi ya mwalimu huyo ambaye amepeleka mganga wa kienyeji kupiga ramli chonganishi nitatoa majibu nakuwaeleza hatua gani zaidi zimechukuliwa”amesema Samizi
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Imenya wameiomba Serikali kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara ili kuwatoa hofu kutokana na kuwepo vitisho vinavyotokana na imani za kishirikiana .
Athony Kija na Suzana Mhoja wamesema mwalimu huyo alisababisha wanakijiji waishi kwa hofu kutokana na mganga aliyempeleka shuleni hapo kuwaambia wanafunzi kuwa wanalogwa na baadhi ya wazazi.