Mmoja aponyoka kunyongwa mauaji ya bilionea Msuya




Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imetengua hatia na adhabu ya kunyongwa dhidi ya Mussa Juma Mangu aliyekuwa amehukumiwa kunyongwa, yeye na wenzake wanne, kwa mauaji ya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, Erasto Msuya maarufu kama Bilionea Msuya.

Mahakama hiyo imetengua hatia na adhabu hiyo dhidi ya Mangu kufuatia rufaa waliyoikata Mangu na wenzake wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyowatua hatiani na kuwahukuku adhabu hiyo.

Hukumu hiyo imesomwa leo Jumatano, April 12, 2023 na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Habert George, kwa njia ya video conference, huku warufani hao wakisikiliza hukumu hiyo wakiwa katika Gereza la Ukonga wanakohifadhiwa.

Mahakama hiyo imetengua hatia na adhabu dhidi ya Mangu baada ya kuridhika kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwa kosa hilo na ikaamuru aachiliwe huru mara moja kutoka gerezani alikokuwa.


Hata hivyo, wakati mahakama hiyo ikimfutia adhabu Mangu na kuamuru aachiliwe huru mara moja, imeamuru wenzake wanne waendelee na adhabu hiyo baada ya kuridhika kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani kwa kosa hilo kama walivyohukumiwa na Mahakama Kuu.

"Rufaa dhidi ya mrufani wa pili Mussa Juma Mangu, imekubaliwa na mahakama hii inaamuru mrufani wa pili, aachiliwe mara moja 
kutoka gerezani. Warufani wengine wote rufaa yao imekataliwa," amesema Naibu Msajili huyo akihitimisha hukumu hiyo.

Wengine waliokuwa wamekatwa rufaa hiyo kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, ambao wamekwaa kisiki ni Sharif Mohamed Athuman, Karim Issa Kihundwa, Sadick Mohamed Jabir na Ally Mussa, maarufu kama Majeshi.

Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa jijini Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai.

Julai 23, 2018, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, katika hukumu iloyotolewa na Jaji Salma Maghimbi, aliyeshikilia kesi hiyo, iliwatia hatiani washtakiwa hao watano na kuwahukuku adhabu hiyo.

Hata hivyo, hukumu hiyo ilimwachia huru mshtakuwa mmoja, Shaibu Said baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha mashtaka dhidi yake.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad