STRAIKA Mzambia Kennedy Musonda, amesema Klabu ya Yanga imemsaidia kuitwa kwenye timu ya taifa kwa mara ya kwanza akiwa kama mchezaji anayesakata soka la kulipwa nje ya nchi, hivyo anajivunia kuwa kwenye kikosi hicho.
Musonda ambaye amesajiliwa kipindi cha dirisha dogo msimu huu akitokea Klabu ya Power Dynamos ya kwao Zambia, alisema alishawahi kuitwa huko nyuma kwenye timu ya taifa, lakini alikuwa ni mchezaji wa timu zinazocheza ndani ya nchi, ila safari hii anacheza soka la kulipwa nje ya nchi.
"Najivunia kuwa kwenye klabu hii kwa sababu imenisaidia kuitwa kwenye timu yangu ya taifa kwa mara ya kwanza nikiwa mchezaji ninayecheza soka la kulipwa nje ya nchi, huko nyuma nilishawahi kuitwa, lakini nilikuwa mchezaji wa ndani, kwa sasa tupo kwenye hali nzuri na kikosi chetu na tunataka kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa sababu tumeshindwa kufanya hivyo kwa miaka ya karibuni.
"Nafikiri Yanga imenisaidia kwa sababu ya hii michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika hatua ya makundi, ni michuano mikubwa watu wengi wanaifuatilia, makocha Yanga wakanipa nafasi na mchango wangu umeonekana, hivyo hakukuwa na njia nyingine kwa wakubwa wa soka Zambia na benchi la ufundi zaidi ya kunijumuisha kwenye kikosi," alisema.
Alisema malengo waliyojiwekea msimu huu ni kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, na kuendelea kufanya vema kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho kiasi cha kuifanya Yanga kuwa moja ya timu tishio barani Afrika.
Awali, straika huyo hakukubalika kwa wapenzi na mashabiki kutokana na kuonekana kutozoea mazingira na pia mfumo, lakini ghafla ameotokea kuwa tishio na kuanza kuwa kipenzi cha baadhi ya mashabiki wa Yanga.