KOCHA Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi ameufuatilia mchezo wao dhidi ya TP Mazembe akiwa kwake Ubelgiji leo wakishinda kwa bao 1-0 lakini akafichua kwamba usiku wa kuamkia jana aliota kuwa mfungaji wa bao hilo ni Farid Mussa.
Yanga imemaliza kibabe mechi za Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiifunga Mazembe kwa mara ya pili na kufikisha jumla ya alama 13 kileleni huku wakisubiri matokeo ya US MONASTIR wanaocheza baadaye dhidi ya Real Bamako ya Mali.
Nabi amesema baada ya kuota ndoto hiyo wakati wa mapumziko alishauriana na wasaidizi wake kumuingiza Farid mwanzo wa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya ambaye alimuona hakuwa katika kiwango bora katika dakika 45 za kwanza.
"Hii ni mara ya pili niliwahi kuota kama hivi kwa Mayele (Fiston) na alifunga ilikuwa msimu uliopita lakini Sasa ni Farid ambaye hata mazoezini kabla ya kuondoka niliona ameongezeka ubora,"amesema Nabi.
"Nawapongeza sana wachezaji wangu na wasaidizi wangu kwa kusimamia malengo ya klabu yetu vizuri, nilitamani sana kushinda mechi hii ni wajibu wetu kuwafanya mashabiki wetu wawe na furaha."
Yanga Sasa inasubiri droo ya hatua ya robo fainali kujua watakutana na timu ipi kati ya USM Alger, Rivers United au Pyramids.