Mwanza. Uongozi wa Kitongoji cha Nyashimbe Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza alipokuwa akiishi Milembe Suleman (41) aliyefariki kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana umesema, kitongoji hicho kitamkumbuka kutokana na michango yake ya kimaendeleo kwenye nzengo.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Aprili 28, 2023 nyumbani kwa Milembe eneo la Nyashimbe Kata ya Usagara wilayani humo, Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Dotto Gabriel amesema marehemu alikuwa akishiriki vizuri shuguli za maendeleo katika kitongoji hicho.
“Michango mbalimbali ya maendeleo, aliwahi kuchangia barabara iliyokatika hapa tulishirikina naye kuweka mulamu na mawe ambapo alitumia gharama zake Sh400,000. Milembe alikuwa hana shida yoyote na jamii ya hapa hata mimi kiongozi nilikuwa nashirikiana naye vizuri tu,”amesema Gabriel
Shemeji wa Milembe, Sospeter Mkakalo amesema familia imepata pigo kuondokewa na mpendwa wao akidai alikuwa tegemeo lao.
“Baada ya kupata taarifa za tukio (za kuawa) tulishtuka sababu hatukutegemea kwamba hili tukio litakuwa hivi na hatukuamini hadi tulipoona mwili wake.
“Katika familia alikuwa ni mtu anayejitoa sana, alikuwa na mchango mkubwa sana kwa ndugu, kwa jamaa, alijitoa kusaidia jamii, kusaidia familia kwahiyo tumempoteza mtu ambaye wa muhimu sana katiak familia,”amesema
Amesema Milembe aliolewa na kubahatika kupata mtoto mmoja wa kike lakini baadaye alitengana na mumewake.