Dodoma. Utekelezwaji wa mradi wa matumizi bora ya nishati hapa nchini utapunguza matumizi ya nishati ambayo siyo ya lazima yaliyokuwa yakimuongezea gharama ya maisha mwananchi
Imeelezwa kuwa Watanzania wamekuwa wakilalamika kutumia uniti nyingi wakati hawakagui vifaa kama friji, taa za nyumbani wanazotumia zinatumia umeme kiwango gani.
Hayo yameelezwa Jumatano, Machi 22 jijini hapa na mratibu wa mradi wa utekelezaji wa matumizi bora ya nishati, Emilian Nyanda wakati akizungumza kwenye kikao cha wadau wa sekta habari kuhusu uelewa wa mradi huo.
Mradi huo ulianza mwaka 2022 na unatarajia kukamilika 2024, unatekelezwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Umoja wa Ulaya (EU).
Nyanda ambaye ni ofisa kutoka Wizara ya Nishati, amesema Watanzania wamekuwa wakilalamika kutumia uniti nyingi za umeme bila ya kukagua vifaa wanavyotumia kama friji, taa zinatumia umeme kwa kiasi gani.
Amesema kupitia mradi huo kutakuwa na vifaa vya umeme vyenye viwango wa matumizi kidogo ya umeme ambavyo vitapunguza matumizi ya umeme na kumpunguzia gharama za maisha mwananchi.
“Kumbe inawezekana vifaa anavyotumia vinatumia umeme mwingi, kutakuwa na balbu yenye matumizi ya chini lakini zinakupa huduma zile zile,”amesema Nyanda.
Amesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa nchini na utasaidia kupunguza nishati ambayo sio ya lazima iliyokuwa ikitumika.
“Kwa mfano kupitia mradi huu tutaweza kama unatumia kilowati 10 kuzalisha kiasi fulani kwa kutumia nishati ikiwemo ya umeme sasa unaweza ukawa unatumia kilowati tano kupata prodact ile ile,”amesema Nyanda.
Mratibu huyo amesema mradi huo unatekelezwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Chuo cha Teknolojia (DIT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Amesema kwa sasa wametafuta mshauri elekezi ambaye anakusanya maoni kuhusu vifaa gani vya umeme vinatumika kwa wingi na wataanza na vitano.
Amesema Aprili 5 mwaka huu mshauri huyo atafanya wasilisho vifaa ambavyo wataanza navyo ambapo wadau watavitaja.
Kwa upande wake Mchambuzi wa kitaifa wa matumizi bora ya nishati, Acfei Maseke amesema Tanzania imeanza kuandaa kiwango cha ubora wa vifaa vya umeme vinavyongia hapa nchini.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kutokana na Tanzania kuwa dampo la vifaa visivyokuwa na ubora, huku akidai Kenya wameweza kulidhibiti jambo hilo na wafanyabiashara wengi wamekuwa wakikimbilia Tanzania.