WAKATI Klabu ya Yanga ikisema itachukua tahadhari zote katika mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili ili kuepuka yasije yakawakuta ya watani wao wa jadi, Simba msimu uliopita dhidi ya Jwaneng Galaxy
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema akipata nafasi ataungana na Watanzania kushuhudia mechi hiyo.
Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, akikabidhi zawadi ya Sh. milioni 10 kwa Yanga jijini Dar es Salaam jana, kutokana na ushindi wao wa mabao 2-0 walioupata ugenini nchini Nigeria dhidi ya Rivers United, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia kwa kila goli litakalofungwa na timu hiyo pamoja na Simba kwenye michuano ya kimataifa, alisema rais amewapongeza kwa ushindi huo na kuahidi bado fedha zipo waendelee tu kutikisa nyavu.
“Leo (jana), nimekuja hapa kutoa pongezi za Rais Samia Suluhu kwa ushindi wa mabao 2-0 na kuwatakia kheri katika mechi ya marudiano dhidi ya Rivers United na kuendelea kuwasisitiza kutikisa nyavu kwa sababu fedha zipo.
"Wachezaji wacheze kwa moyo kwa sababu wanaitangaza Tanzania na amesema kama ratiba zake zitaenda vizuri basi atakuwa sehemu ya Watanzania watakaoshuhudia Yanga ikimfunga Rivers United katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na [timu ya] Tanzania kuwa sehemu ya zitakazocheza nusu fainali,” alisema Msigwa wakati akikabidhi kitita hicho.
Aidha, akawapongeza wasemaji wa klabu hizo mbili kwa kuwa licha ya mechi kuchezwa uwanjani, lakini pia inachezwa mdomoni kwa sababu ya kuuzungumza mpira.
Alisema kitendo cha kutengeneza maneno vizuri, wanahamasika watu wengi ikiwamo mashabiki na viongozi wa serikali kujikita zaidi katika mpira na kuendeleza sera za Rais Samia katika sekta ya michezo.
Hata hivyo, licha ya Yanga kuwa na faida ya mabao 2-0 dhidi ya Rivers United ugenini, imesema wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa na hawataki kuona makosa kama ya Simba ya kuondolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita na Jwaneng Galaxy ya Botswana, yakitokea kwao.
Oktoba 17, 2021, Simba ikiwa ugenini nchini Botswana kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika raundi ya kwanza, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wao, Jwaneng Galaxy, kabla ya Oktoba 24, mwaka huo kushangazwa katika mchezo wa marudiano Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kipigo cha mabao 3-1, hivyo matokeo ya jumla kuwa 3-3, lakini ikatupwa nje kwa faida ya bao la ugenini na kuangukia Kombe la Shirikisho.
Kutokana na Yanga nayo kupata matokeo kama hayo ya Simba ugenini, lakini yenyewe ikiwa ni kwenye Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali, imeshtuka na kusema itachukua tahadhari kubwa wakikumbuka kilichowakuta watani wao wa jadi.
Katika mchezo huo wa mkondo wa pili dhidi ya Rivers United ya Nigeria, Yanga inahitaji sare yoyote ama ushindi ili kutinga hatua ya nusu fainali.
Akizungumza na Nipashe jana, Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, alisema mechi yao ya marudiano itakuwa ni ngumu na ushindani mkubwa kwa sababu soka ni dakika 90.
Alisema wamefanikiwa kupata ushindi wa maboa 2-0 dhidi ya Rivers United ugenini na kwamba ni matokeo mazuri, lakini wanahitaji kuingia katika mchezo huo kwa nidhamu na tahadhari kubwa kwa sababu ya kutotaka ya mwaka 2021 kujirudia kwao.
“Jumapili tunaipeleka nchi nusu fainali ya Afrika, tuna matokeo ya mabao 2-0 mkononi, lakini bado tuna kazi kubwa mechi ya marudiano hatutaki kuona ya Jwaneng Galaxy ilivyowatoa wenzetu hapa nyumbani," alisema Kamwe.
Kamwe pia, alisema timu zote mbili [Simba na Yanga], kufika hatua ya robo fainali moja ya kitu kilichochangia ni pamoja na hamasa kutoka kwa Rais Samia kwa uamuzi wake wa busara wa kutoa Sh. milioni tano kwa kila bao linalofungwa na timu hizo kimataifa.