Mwanza. Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini matumizi ya jumla ya Sh11.78 bilioni bila nyaraka toshelevu katika mamlaka za halmashauri 111 nchini.
Katika ripoti yake iliyowasilishwa bungeni leo Alhamisi Aprili 6, 2023, CAG pia amebaini kuwa halmashauri 71 zililipa Sh10.08 bilioni bila kudai risiti za EFD huku halmashauri zingine 40 zikibainika kulipa Sh1.70 bilioni bila nyaraka husika.
Ripoti hiyo ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/22 imebaini halmashauri tisa kutumia Sh898.85 milioni kwa matumizi yasiyo na manufaa, kati ya fedha hizo, Sh322.29 milioni zilitumika halmashauri ya Jiji la Arusha.
Baadhi ya halmashauri pia zimebainika kufanya manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa barabara ambavyo hata hivyo uwezo wake haukuweza kuthibitishwa.
Taarifa ya CAG Charles Kichere ambayo imewasilishwa bungeni baada ya kupokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan Machi 29, 2023 imebaini halmashauri 71 kulipa Sh7.7 bilioni kutoka kwenye akaunti za amana kinyume na madhumuni ya fedha na bila kupata idhini ya mamlaka husika.
Ukaguzi huo pia umebaini kuwa halmashauri 14 zililipa Sh1.51 bilioni kwa ajili ya huduma na bidhaa kwa kutumia fedha taslimu kinyume na Kanuni za ununuzi.
“Kutumia pesa za umma bila maelezo au viambatisho vya kutosheleza kunatia shaka juu ya uhalali wa malipo hayo," inasema sehemu ya taarifa ya CAG
Kuhusu tathmini ya taarifa za mfumo wa mapato (LGRCIS), CAG amebaini mapato ya Sh11.07 bilioni yalikusanywa kutoka vyanzo vya mapato kwa kutumia mashine za POS lakini hayakupelekwa kwenye akaunti za benki za Mamlaka za Serikali za Mitaa husika.
“Makusanyo ya mapato kupitia LGRCIS yalibaini mapato ya Sh76.59 bilioni hayakukusanywa, hususani yatokanayo na tozo za vizimba vya masoko, uuzaji wa viwanja, mazao ya kilimo, leseni za vileo, ushuru wa uchimbaji wa vifaa vya ujenzi, leseni ya biashara, ushuru wa huduma na ushuru wa kupangisha maduka na nyumba katika stendi za mabasi na masoko ya Halmashauri,” anasema CAG katika taarifa yake
Taarifa hiyo imebaini kutokusanywa kwa mapato kutoka kwa wadaiwa waliopewa hati za madai za mfumo wa mapato (LGRCIS) huku mapato ya Sh4.94 bilioni zilizokusanywa na mawakala wa ukusanyaji mapato hazikuwasilishwa kulingana na makubaliano ya mikataba.