Sabaya akiri makosa, aachiwa kwa masharti




Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, imemuachia kwa masharti ya kutofanya kosa la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja na kulipa fidia ya Sh5 milioni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya baada ya kukiri kosa la kula njama na kuzuia utekelezaji wa haki na kosa la pili kudhania madaraka ambayo si yake

Hukumu hiyo imetolewa leo Aprili 5, 2023 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Salome Mshasha baada ya kumtia hatiani Sabaya aliyekiri kutenda makosa hayo.

Sabaya na wenzake wakiwa eneo la Mboso lililoko Kata ya Masama wilayani Hai bila kufuata sheria walifanya upekuzi nyumbani kwa mfanyabiashara Alex Swai na kujipatia Sh50 milioni kinyume cha sheria

Kosa la pili Sabaya na wenzake katika maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro na Arusha, kwa nia ovu walimkamata Swai kwa madai ya kukwepa kodi ambapo kisheria hawakuwa na mamlaka hayo.


Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Sabaya anayetetewa na mawakili Moses Mahuna na Hellen Mahuna, alikiri kutenda makosa hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Salome Mshasha na hivyo mahakama ikamtia hatiani kwa makosa hayo.

Katika hukumu hiyo, Hakimu Mshasha alimwamuru Sabaya kulipa fidia ya Sh5 milioni kwa Elibariki Swai ambaye ni ndugu na Alex Swai na pia akamwamuru Sabaya kuhakikisha hafanyi kosa lolote la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Awali Sabaya alisomewa mashtaka yake na alikiri kutenda makosa hayo na hakimu alimhukumu kulingana na makubaliano (Plea bargaining) aliyoingia na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ambaye alimfutia mashtaka ya uhujumu uchumi.


Baada ya kesi hiyo ya awali namba 2/2022 kufutwa na Hakimu Mshasha, mwendesha mashitaka ambaye ni wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Veridiana Mlenza alimsomea Sabaya mashtaka mapya mawili.

Awali katika kesi hiyo namba 2/2022, ilikuwa na jumla ya makosa saba na washtakiwa watano ambapo Sabaya mwenyewe alikuwa na mashtaka matano kabla ya kesi hiyo kufutwa jana na kufunguliwa kesi mpya ya jinai.

Akimsomea mashtaka hayo ambayo ni sehemu ya makubaliano na DPP, wakili Mlenza amesema Januari 19,2021, Sabaya na washirika wake wanne ambao tayari walishatiwa hatiani mwaka jana, walijipa mamlaka wasiyostahili.

Baada ya kukamilika kwa mchakato huo, saa 9 alasiri Sabaya alitoka chumba cha mahakama akiwa amefuatana na askari polisi na kupanda gari aina ya Toyota Alphard na kuondoka katika eneo la mahakama akiacha karandika la Magereza.


Taarifa zilizopatikana zilisema alipelekwa polisi kwa taratibu za kuachiwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad