Sakata mwili uliorudishwa kituo cha polisi lachukua sura mpya



Geita. Kutokana na shinikizo ili kujiridhisha na sababu za kifo cha kijana Enos Misalaba aliyefariki dunia Machi 28, 2023 katika Kituo cha Afya Mganza, alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua mahabusu, mwili wake umerudiwa kufanyiwa uchunguzi kabla ya kwenda kuzikwa.

 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Berthaneema Mlay amesema wamelazimika kuufanyia mwili huo uchunguzi upya ili kujiridhisha sababu za kifo chake na baadaye wataupeleka makaburini kwa ajili ya maziko.

Mazishi hayo yatafanywa na familia kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya na Jeshi la Polisi.

“Hali huku ni tulivu tunajiandaa kuuhifadhi mwili wa huyu kijana na sasa tupo kwenye mchakato wa kurudia ‘post mortem’ ili tuweze kuuhifadhi mchana. Tunajaribu kuona hali inakuwa nzuri ili tuweze kuhifadhi mwili wa huyo kijana,” amesema.


Alisema hadi saa hakuna anayeshikiliwa kwa tukio hilo na kwamba baada ya maziko polisi watafanya upelelezi ili kuwapata waliohusika na tukio hilo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumzia malalamiko dhidi ya polisi wanaodaiwa kumpiga kijana huyo na tuhuma za uonevu dhidi ya wananchi Kaimu Kamanda amesema, “Tuhuma zinahitaji uchunguzi ili kuhakikisha anayetuhumiwa kweli ni mhusika. Jeshi la Polisi tumeanza hatua, tumefungua jalada la uchunguzi ili tuone kama kweli vijana wetu walihusika au kuna mtu mwingine au kuna sababu zilizochangia tukio hilo kutokea,” amesema Kaimu Kamanda.

Amesema vurugu zilizotokea jana zilisababishwa na vijana wa bodaboda ambao walibeba mwili uliokuwa tayari kwa ajili ya maziko na kusababisha vurugu zilizopelekea kituo cha polisi kuchomwa na baadhi ya watu kujeruhiwa.

Machi 30 wananchi walikataa kuuzika mwili wa Enos Misalaba baada ya msomaji risala ya marehemu kudai alifariki kwa kuugua kifua, kitendo kilichopingwa na waombolezaji walioamua kurudisha mwili kituo cha Polisi na badaye kuzuka vurugu baina ya wananchi na polisi.

Hali hiyo ilisababisha askari kutumia mabomu ya machozi kuwatuliza na vurugu hizo zilisababisha kituo cha polisi kuchomwa moto.

Wananchi wa eneo hilo wanapinga uonevu unaofanywa na askari polisi wa kituo hicho wanaodaiwa kumkamata mtuhumiwa na kumpiga kitendo kinachodaiwa kusababisha kifo chake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad